Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba amekutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia Mhe. Pahala Mansury jijini Jakarta, ikiwa ni hatua za mwisho za maandalizi ya Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakayofanyika kuanzia tarehe 24-26 Januari, 2024 nchini humo.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejiridhisha na maandalizi yanayoendelea ikiwemo ukamilishwaji wa hati saba za ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali zinazotarajiwa kusainiwa wakati wa ziara hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Waziri Makamba amesema ziara hiyo ni muendelezo wa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Indonesia ambao mwaka huu unatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.
Ameongeza kuwa ziara hiyo pia inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Indonesia katika maeneo ya kımkakati ya biashara, uwekezaji, afya, elimu, uchumi wa buluu na kilimo.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia Mhe. Pahala Mansury amesema Indonesia iko tayari kumpokea Mhe. Rais Samia nchini mwao na kusisitiza kuwa Indonesia inathamini uhusiano wake na Tanzania na itaendelea kushirikiana kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Indonesia Mhe. Makocha Tembele na Mkurugenzi wa Afrika Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia
Tanzania na Indonesia zimekua na uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu tangu miaka ya 60, ambapo uhusiano ulijikita kwenye masuala ya ushirikiano baina ya nchi za Asia na Afrika ulioasisiwa na Mkutano wa Bandung mwaka 1955.
Kwenye awamu ya sita ya uongozi wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameimarisha zaidi uhusiano huu kwa kuelekeza nguvu zaidi kwenye kuongeza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili.
Tanzania inaitazama Indonesia kama nchi rafiki wa muda mrefu , lakini pia kama lango la kufungua fursa nyingi zaidi za kibiashara baina yake na nchi za eneo la ukanda wa Kusini Mashariki mwa bara la Asia.
Mhe. Rais Samia anatarajiwa kuwasili kwa ziara hiyo ya Kitaifa nchini Indonesia kuanzia tarehe 24 Januari 2024.