Na Sophia Kingimali.
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amewataka Wakala wa Barabara nchini (TANROAD) kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye kingo za madaraja hasa katika kipindi hiki cha mvua lakini pia wahakikishe wanakuja na mpango wa muda mrefu wa kutengeneza njia sahihi maji.
Maagizo hayo ameyatoa leo januari 22,2024 jijini Dar es salaam wakati akitembelea maeneo yaliyoathirika na mvua hizo katika eneo la jangwani na daraja kunduchi.
Amesema kufuatia mvua zinazoendelea kunyeesha ni vyema wakawa wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara hasa kwenye maeneo ya madaraja ili waweze kutoa alama za taadhari ili kuwasaidia wananchi pindi athari zinapotokea zisiathiri watu na vyombo vya usafiri.
“Nyinyi Tanroad ndio wenye kujua changamoto na viashiria vya hatari sasa ni vyema muwe mnafanya ukaguzi ili mtoe tahadhari ya haraka kwa wananchi kuepuka madhara kama haya yaliyojitokeza”Amesema.
Aidha ametoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki wanapopita kwenye maeneo ya madaraja wakiona maji mengi na sehemu ya ardhi haionekani kuacha kupita na kusubiri maji yapite kwanza.
Sambamba na hayo ameishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha huduma za miundombinu zinarejea kwa haraka katika maeneo yote yaliyoharibika.
“Nipongeze sana serikali ya awamu ya sita chini ya jemedari wetu Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake pindi mamlaka ya hali ya hewa(TMA) kutangaza uwepo wa mvua hizi kubwa alitoa maelekezo kwa wizara zote kujiandaa na kukabiliana na changamoto zozote zitakazotokea ndio maana unaona changamoto hii ilipotokea wenzetu TANROAD makao makuu na mkoa wameshughulikia hizi changamoto kwa haraka”amesema.
Amesema pamoja na kujitahid kutatua changamoto kutokana na mabadiliko ya tabia nchi wanapaswa kujiandaa vizuri ikiwa ni pamoja na kueweka kingo ili kuhakikisha maji hayawi tena tatizo la kuharibu miundombinu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya Kinondoni Saad Mtambule ameipongeza TANROAD na TARURA kwa jitihada kubwa waliyoofanya kwa kurudisha huduma ya usafiri katika jiji la Dar es salaam.
Aidha ametoa rai kwa wananchi kuchukua taadhari kubwa pindi mvua zinaponyeesha kwa kuepuka kupita kwenye madaraja yaliyojaa maji.
Naye,Muhandisi Suzana Lukasi amesema mvua imeharibu miundombinu ya madaraja na barabara lakini juhudi kubwa imefanyika ya kuhakikisha miundombinu hiyo inarejeshwa kwa wakati.
“Mvua hizi zilizonyeesha zimesababisha uharibifu mkubwa lakini tumejitahidi kuhakikisha miundombinu hiyo tunairekebisha na sasa tumefungua njia zinapitika huku ukarabati mwingine unaendelea”amesema Mha Suzana.
Ziara ya Naibu waziri wa ujenzi inaendelea kuhakikisha anakagua miundombinu yote iliyoharibika na kuangalia hatua zilizochukuliwa.