Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francis amemwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Vatican tarehe 11 – 12 Februari, 2024.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) alipozungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri Makamba ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Vatican, atakuwa na mazungumzo na Baba Mtakatifu Papa Francis pamoja na Katibu wa Vatican, Mhe. Pietro Parolin. Uhusiano kati ya Tanzania na Vatican ulianza miaka ya 1960 wakati ambapo Vatican ilianzisha Ubalozi wake hapa nchini.
Tangu wakati huo Vatican kupitia Kanisa Katoliki imekuwa mstari wa mbele katika kujishughulisha na masuala ya kiroho, amani, elimu na program za afya. Kwenye ziara hiyo Mhe. Rais Samia ataongozana na wawakilishi watano wa waumini wa Kanisa Katoliki Tanzania kutoka kwenye jumuiya mbalimbali za kanisa hilo.
“Vatican kupitia Kanisa Katoliki limechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya elimu kabla na baada ya uhuru wa Tanzania Bara kwa kutoa elimu kwa Watanzania wa dini zote. Kupitia shule na vyuo mbalimbali Kanisa kwa kushirikiana na Serikali limechangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha viongozi na wataalam mahiri kwenye maeneo mbalimbali,” alieleza Waziri Makamba.
Katika ziara hiyo Tanzania inaangalia fursa za kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano yatakayotoa msukumo mkubwa zaidi kwenye kuimarisha na kukuza amani na usalama.