Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mh. Haroun Ali Suleiman Mkutano wa Wadau uliojadili Rasimu za Miswada ya Sheria ya Usuluhishi na Sheria ya kuanzisha Kituo cha Usuluhishi wa Migogoro Zanzibar ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege.
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji akiwakaribisha Wadau katika Mkutano wa kujadili Rasimu za Miswada ya Sheria ya Usuluhishi na Sheria ya kuanzisha Kituo cha Usuluhishi wa Migogoro Zanzibar ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege.
Wadau mbali mbali walioshiriki katika Mkutano wa kujadili Rasimu za Miswada ya Sheria ya Usuluhishi na Sheria ya kuanzisha Kituo cha Usuluhishi wa Migogoro Zanzibar ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege.
………..
Na Faki Mjaka.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mh. Haroun Ali Suleiman amesema kuanzishwa kwa Sheria ya Usuluhishi na Kituo cha Utatuzi wa Migogoro Zanzibar kutaongeza imani ya wawekezaji kuja nchini kuwekeza miradi yao ya kimaendeleo.
Amesema kituo hicho kitakapoanzishwa kitawahudumia wenyeji na wageni na hivyo kupunguza kasi ya watu kuepelekana mahkamani hasa pale migogoro ya kibiashara na uwekezaji inapotokea.
Waziri Haroun aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege alipofungua Mkutano wa Wadau uliojadili Rasimu za Miswada ya Sheria ya Usuluhishi na Sheria ya kuanzisha Kituo cha Usuluhishi wa Migogoro Zanzibar uliohudhuriwa na wadau kutoka sekta mbali mbali nchini.
Alisema hali ya Zanzibar kiuchumi inaimarika sana kutokana na juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi za kuwavutia Wawekezaji kuwekeza miradi yao ya kiuchumi Zanzibar.
Alisema suala la uwekezaji linahitaji pia kuwa na sheria nzuri ili kuwavutia wengi zaidi kuja kuwekeza nchini na kuleta tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Alifahamisha kuwa, waligundua kwama, Sheria iliyopo kwa sasa ya utatuzi wa migogoro imepitwa na wakati na hupelekea migogoro mingi ambayo huchukua muda mrefu na gharama kubwa mahkamani.
Alisema Serikali kwa makusudi imeamua kuanzisha Kituo maalum cha usuluhishi wa migogoro ambacho kitakuwa na jukumu la kuipatia ufumbuzi migogoro itakayojitokeza.
“Badala watu kupelekana Mahkamani panapotokea mgogoro sasa watu watakuwa wanaenda katika kituo hicho kwa ajili ya kutafuta suluhu, na imani yetu watakaokwenda kituoni watatoka hapo kila upande ukiwa umeridhika” Alifafanua Waziri Haroun.
Aliongeza kuwa, Kituo hicho kitakuwa chini ya Mwenyekiti wake (atakayeteuliwa na Rais), ambaye pia atakuwa na jukumu la kutumia busara kwa kushirikiana na Wajumbe wake kuitatua migogoro itakayofikishwa katika kituo hicho.“Ukweli ni kwamba Wawekezaji hupenda mazingira salama ya uwekejazi wao.
Wanapopelekwa mahkamani, huvunjika moyo na kutafuta nchi nyingine zenye mazingira rafiki ya uwekezaji wao, ili yasifikie hayo Kituo hiki kitakuwa kichocheo cha kuwaongezea Imani na usalama wao” Aliongeza Waziri Haroun.
Akitoa historia ya chimbuko la uwamuzi huo, Waziri Haroun alisema, Rais Dkt. Mwinyi baada ya kuingia madarakani aliagiza sheria zote zilizopitwa na wakati zifanyiwe marekisho au kufutwa na kutungwa upya.
Miongoni mwa Sheria hizo ni sheria ya usuluhishi ambayo ilitungwa toka zama za wakoloni mwaka 1926 hivyo ni wajibu kufutwa ili kuendana na hali halisi ya sasa.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mwanasheria Mkuu Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji alisema ni muda muafaka wa Zanzibar kuwa na kituo chake cha usuluhishi wa migogoro hasa kutokana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kushajihisha Uchumi wa Buluu na uwekezaji wake.
Alisema Rasimu mbili zilizokuwa zinajadiliwa zitatoa Dira muhimu na mustakabi mwema wa Zanzibar ambapo shughuli za uwekezaji zitakapoongezeka, zitawanufaisha wananchi kwa ujumla wake.
Alifahamisha kuwa, kiutaratibu Rasimu hiyo itapelekwa katika kamati ya uongozi ya Wizara na baadaye kikao cha Makatibu wakuu kabla ya kupelekwa Baraza la Wawakilishi kwa hatua za kujadiliwa zaidi.
Amesema kukamilika kwa Sheria na Kituo hicho cha usuluhishi kutachochea imani zaidi kwa wawekezaji kwamba Zanzibar ni sehemu nzuri ya uwekezaji na hivyo kupelekea kutekeleza dhamira ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kuifungua Zanzibar kiuwekezaji hasa katika uchumi wa Buluu.
Akichangia katika mkutano huo, Mwenyekiti mstaafu wa tume ya kurekebisha sheria Zanzibar ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Jaji Mshibe Ali Bakari amesema moja ya faida ya Kituo hicho ni kuipunguzia mzigo mkubwa Mahkama kwani migogoro mingi itapatiwa ufumbuzi katika kituo hicho badala ya mahkamani.
Kwa upande wake Rais mtaafu wa Jumuiya ya Mawakili Zanzibar na Wakili wa kujitegemea Slim said Abdala amesema uzoefu unaoenesha kuwa migogoro ya kibiashara na uwekezaji haitakiwi kwenda katika Mahkama za kawaida, bali hupelekwa katika Vituo vya usuluhishi.
Amesema Kituo cha usuluhishi ni sehemu muafaka zaidi kwa vile ni maamuzi hutolewa kwa haraka zaidi na kwa ufanisi bila kuvutana katika mahkama kunakochukua muda mrefu na gharama kubwa.
Wakili Slim aliahidi kuwa wapo tayari kuunga mkono kituo hicho ambacho ana Imani kitazidi kuchochea kasi ya uwekezaji na maendeleo nchi.