Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres baada ya kufanya mazungumzo kando ya Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi na Serikali Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) ulioanza tarehe 15 – 20 Januari, 2024, Kampala – Uganda. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Umoja wa Mataifa (UN) umeahidi kuimarisha kitengo cha maafa nchini pamoja na kuwaongezea watumishi uwezo na ujuzi wa uokoaji.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo jana jioni baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa UN Mheshimiwa Antonio Gutteres Kampala, Uganda.
Waziri Mkuu yuko nchini Uganda akimwakilisha Rais Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi na Serikali Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) uliomalizika jana pamoja na mkutano wa Tatu wa Kusini wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la G77 na China unaoanza leo.
Alisema katika mazungumzo yao na Mheshimiwa Gutteres pamoja na mambo mengine alimuelezea kuhusu maafa yaliyotokea wilayani Hanang mkoani Manyara.
Desemba 3, 2023 wilaya ya Hanang ilikumbwa na mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu 89, majeruhi 139 na nyumba 261 ziliathiriwa, pia miundombinu mingine kama ya barabara, maji, umeme nayo iliharibika.
Mheshimiwa Majaliwa alimueleza kiongozi huyo namna ambavyo kamati ya kitaifa inavyoshughulikia maafa yanapotokea na ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuwaongezea uwezo watumishi wa kitengo hicho.
Pia, Waziri Mkuu amesema mbali na maafa ya Hanang pia wamezungumzia suala la wakimbizi na ameipongeza Tanzania kwa kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi.
Amesema kiongozi huyo ameahidi kushirikiana na Tanzania kuwahamisha wakimbizi ambao nchi zao kwa sasa zina amani waweze kurejea makwao.
Alisema wakimbizi hao wanahamasishwa kurudi nchini kwao kwenda kushirikiana na wenzao kujenga uchumi wa mataifa yao. UN itahudumia urejeaji kwenye nchi zao.
Alisema kiongozi huyo ameishukuru Tanzania kwa namna inavyojitoa katika kusaidia mataifa mengine ikiwemo kutoa askari wake kushiriki katika ulinzi wa amani kimataifa.