Muonekano wa barabara ya lami ya Kifagilo-Magingo katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 95.
Kaimu meneja wa Tarura wilaya ya Songea Mhandisi Davis Mbawala kushoto,akizungumza na baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Madaba juu ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kifagilo-Magingo ambayo ujenzi wake unaendelea.
Kaimu meneja wa Tarura wilayani Songea Mhandisi Davis Mbawala wa pili kulia,akiwawaelekeza jambo baadhi ya wakazi wa Madaba kuhusu maendeleo ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kifagilo-Magingo inayojengwa kwa lengo la kuboresha miundombinu ya barabara katika mji wa Madaba.
…..
Na Mwandishi Maalum, Madaba
BAADHI ya wananchi wa Halmashauri ya Madaba wilayani Songea,wameiomba serikali kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kujenga barabara za lami za mitaa zitakazowavutia watu wengi hasa wafanyabiashara kwenda kuwekeza katika Mji mdogo wa Madaba.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema,Halmashauri ya Madaba bado iko nyuma kimaendeleo kwa sababu ya kukosekana kwa huduma muhimu ikiwemo barabara za lami,maji na umeme wa uhakika.
Onesmo Ngole alisema,hali ndiyo inayosababisha wafanyabiashara kutokwenda kuwekeza licha ya kuwa na rasilimali kubwa ya ardhi,mito mingi na watu wenye uwezo wa kufanya kazi za kujitolea na zile za kujipatia kipato.
Silvanus Mwenda mkazi wa kijiji cha Lituta,ameipongeza Tarura kuanza kujenga barabara za lami za mitaa kwani zitasaidia kupandisha hadhi ya Halmashauri na makazi yao.
Hata hivyo,ameomba barabara hiyo kuunganishwa kwa lami hadi katika Hospitali ya Halmashauri ili kuwaondolea adha ya usafiri watu wanaokwenda kupata matibabu katika Hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenda,barabara hiyo imesaidia kupandisha thamani ya maeneo yao tofauti na hapo awali ambapo nyakati za kiangazi kulikuwa na vumbi na masika kuwa na tope,hivyo kushindwa kupitika kirahisi.
Aidha,ametaka kazi ya kufunga taa za barabarani na ujenzi wa mifereji ufanyike haraka ili waweze kutumia barabara hiyo hata saa za usiku kwa ajili ya kufanya biashara ndogo ndogo.
“ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami na uwekezaji wa taa utapunguza hata matukio ya watu kuporwa vitu nyakati za usiku na vijana wa mitaani kutokana na giza lililopo katika eneo hili”alisema Mwenda.
Kwa upande wake Mhandisi wa barabara kutoka ofisi ya meneja wa Tarura wilaya ya Songea Davis Mapunda alisema,serikali imeanza kujenga barabara za lami za mitaa katika Halmashauri ya Madaba.
Alisema,ujenzi wa barabara za lami katika Halmashauri hiyo ni pango maalum wa serikali ili kushawishi na kuvutia watu wengi kwenda kuwekeza miradi mbalimbali na kurahisisha mawasiliano kwa wananchi.
Alisema, Tarura imeanza kujenga barabara ya Kifagilo-Magingo yenye urefu wa kilomita 1.1 kwa gharama ya Sh.milioni 593.6 ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wanaotoka maeneo yao kwenda makao makuu ya Halmashauri kwa ajili ya kufuata huduma.
Alisema,ujenzi wa babara hiyo ulianza mwezi Agosti 2023 na inatarajia kukamilika mwezi Machi 2024 na ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 90 na imeanza kutumika.
Mbawala ametaja kazi zilizobaki katika ujenzi wa barabara hiyo, ni ufungaji wa taa za barabarani na ujenzi wa mitaro ya kupitisha maji na mpango wa Tarura ni kuendelea kuboresha barabara za Halmashauri ya Madaba kwa lami na changarawe kadri fedha zitakapopatikana.