*Rais Museveni ayataka mataifa tajiri yakuze uchumi wa mataifa yanayoendelea
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Wakuu wa Nchi na Serikali Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) katika mkutano wa 19 uliomalizika jana Januari 20, 2024, Kampala, Uganda pamoja na mambo mengine wamekubaliana kuhakikisha wanaimarisha uwekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda ili kukuza uchumi.
Waziri Mkuu ambaye anamwakilisha Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyasema hayo jana Jumamosi, Januari 20, 2024 mjini Kampala, Uganda baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi na Serikali zisizofungamana na Upande wowote (NAM) ulioanza tarehe 15 – 20 Januari, 2024. Katika mkutano huo Rais wa Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museven alikabidhiwa uenyekiti wa NAM.
“…Kwenye uchumi bado nchi wanachama tumesisitizwa uwekezaji kwenye viwanda, uwekezaji kwenye kilimo, uwekezaji kwenye maeneo yanayoweza kuboresha uchumi na hasa kuhamasisha wafanyabiashara wa ndani ya nchi hizo kujenga mahusiano na wafanyabiashara wa mataifa mengine kwa lengo la kuinua uchumi ili kujijenga zaidi.”
Akizungumzia kuhusu masuala ya kijamii, Waziri Mkuu alisema nchi hizo zimekubaliana kuendelea kuzihamasisha jamii zao ziendelee kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii zikiwemo za kujenga uchumi, kulinda ulinzi na usalama katika maeneo yao na pale linapotokea wahakikishe wanayamaliza wenyewe ndani ya nchi zao.
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema katika mkutano huo wamekubaliana namna ya kushughulikia masuala ya kisiasa. “Kuhusu masuala ya kisiasa tumehitimisha kwa kutoa wito kwa nchi wanachama kila nchi ambayo imeweka utaratibu wake kisiasa waendelee na panapotokea kuwa na matatizo ya kisiasa basi waendelee kuyatatua matatizo yao kwa kukaa kwenye meza ya mazungumzo na kuyamaliza.”
Kwa upande wake, Rais wa Uganda na Mwenyekiti wa NAM, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museven aliyataka mataifa yaliyoendelea yashiriki katika kukuza uchumi wa nchi zinazoendelea kwa kununua bidhaa kutoka katika nchi hizo pamoja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za uwekezaji, viwanda na biashara.
“Wanachama wa NAM pamoja na changamoto za kimaendeleo zilizopo bado tunanafasi ya kuzikabili sisi wenyewe kwa kusaidiana katika masuala mbalimbali ikiwemo kufanya biashara baina yetu kwa kununua bidhaa kutoka kwenye nchi zetu kwani tunaidadi kubwa ya watu. Pia tuendelee kuweka mipango ya kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuboresha miundombinu ya barabara, reli, usafiri wa anga ili kurahisha ufanyaji biashara.”
Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Antonio Gutteres alitoa wito kwa mashirika ya kimataifa na nchi zilizoendelea kuwa na mpango endelevu wa misamaha ya madeni kwa nchi za Afrika ili ziweze kuwa na maendeleo endelevu kwenye sekta za elimu, afya, nishati ya umeme pamoja na kukabialiana na baa la njaa.
Kadhalika, Mheshimiwa Gutteres amezitaka nchi za magharibi ambazo ziliahidi kutoa fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi za Afrika zinazokabiliwa na mabadiliko ya tabia nchi zitoe fedha hizo na ameyataka mataifa wanachama wa NAM kuzikumbusha nchi hizo kutoa fedha hizo ndani ya mwaka huu.
Mkutano huo wa siku mbili ulianza Ijumaa, Januari 19, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Ruwenzori, Speke Resort Kampala nchini Uganda. Mkutano wa NAM hufanyika kila baada ya miaka mitatu na Mkutano wa mwisho, wa 18 ulifanyika jijini Baku nchini Azerbaijan mwezi Oktoba, 2019. Mkutano huo haukuweza kufanyika tangu mwaka 2019 kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19 lililoikumba dunia.
Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kwenye masuala ya biashara, uwekezaji, kutokomeza umaskini, mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama katika mipaka, sekta ya afya, mandeleo endelevu, na uchumi wa kidijiti.
Umoja huo ulianzishwa wakati wa enzi za vita baridi ili kusaidia nchi wanachama wake kutoka mabara ya Asia, Afrika na Latin Amerika kuondokana na ukoloni ili kuweza kujitawala kisiasa, kiuchumi na kijamii.