Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akitoa maelekezo alipotembelea eneo la Mto Zira katika Kijiji cha Ifumbo wilayani Chunya mkoani Mbeya ili kukagua hali ya mazingira ya mto huo unaokabiliwa na changamoto za kimazingira kutokana na uchimbaji wa madini uliofanyika.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa katika ziara ya kutembelea eneo la Mto Zira katika Kijiji cha Ifumbo wilayani Chunya mkoani Mbeya ili kukagua hali ya mazingira ya mto huo unaokabiliwa na changamoto za kimazingira kutokana na uchimbaji wa madini uliofanyika.
Sehemu ya Mto Zira katika Kijiji cha Ifumbo wilayani Chunya mkoani Mbeya ambao unakabiliwa na changamoto za kimazingira kutokana na uchimbaji wa madini uliofanyika ambapo Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametembelea eneo hilo na kutoa maelekezo ya Serikali.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na viongozi mbalimbali wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua shughuli za uchimbaji wa dhahabu wilayani Chunya mkoani Mbeya.
……………………..
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaelekeza wawekezaji wote nchini kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kabla ya kutekeleza mradi wowote ili kulinda mazingira.
Pia, amewataka wachimbaji wa madini waliopata leseni za uchimbaji kutoka mamlaka husika kuanza zoezi la kufanya tathmini hiyo ili iwaelekeze namna ya kufanya shughuli zao bila kuathiri mazingira.
Ametoa maelekezo hayo alipotembelea eneo la Mto Zira katika Kijiji cha Ifumbo wilayani Chunya mkoani Mbeya ili kukagua hali ya mazingira ya mto huo unaokabiliwa na changamoto za kimazingira kutokana na uchimbaji wa madini uliofanyika.
Dkt. Jafo amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha Kampuni ya G & I Tech Limited ambayo imekuwa ikichimba dhahabu katika eneo hilo inafanya tathmini hiyo.
Amemtaka mwekezaji huyo kukamailisha mchakato wa TAM ambao utaainisha nini anachopaswa kufanya katika shughuli zake ikiwemo uchakati wa mchanga ufanyike nje ya mto na si ndani kwani kitendo hicho kinachangia uharibifu wa mazingira ya mto.
Pia, ameelekeza itumike teknolojia mbadala ya uchimbaji wa dhahabu ndani ya mto huo kuvuna dhahabu huku akishauri utungwe mwongozo wa usafishaji wa mito katika eneo hilo ili kuepusha uharibifu wa kingo za mto na mazingira kwa ujumla.
“Hatutaki kuzuia wawekezaji na tunatambua Serikali imeendelea kufungua milango ya uwekezaji ili kukuza uchumi lakini wawekezaji hao wanapaswa kuzingatia Sheria ya Utunzaji na Hifadhi ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake ili kunusuru mazingira,“ amesisitiza Dkt. Jafo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera amesema Mto Zira ni msaada mkubwa kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo hivyo unapaswa kutoharibiwa mazingira yake.
Amesema kuwa wawekezaji wakiwekeza katika teknolojia tutafanikiwa na madini yataendelea kupatikana lakini uchimbaji ukifanyika kienyeji kutakuwa na athari.
Mkuu wa Mkoa Homera ameongeza kuwa Serikali inatamani na kuthamini wawekezaji kwani wakiendelea kuwekeza inapata mapato, vijana wanapata ajira.
Naye Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria NEMC Dkt. Thobias Mwesiga amesema hatua za kufanya TAM kwa mwekezaji huyo zinaendelea kwa lengo la kumuwezesha aendelee na uchimbaji.
Amesema kuwa ni kweli shughuli za uchimbaji zinaweza kufanyika popote lakini kinachoangaliwa zaidi ni uzingatia wa sheria ili tujue ni madhara na maslahi yapi yatapatikana kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya uwekezaji.
Halikadhalika, Dkt. Mwesiga ameongeza kuwa kuna kipengele cha kuwashirikisha wananchi kwa asilimia zote kwenye tathmini ya athari kwa mazingira ili kuhakikisha shughuli zinafanyika bila kuathiri mazingira.