Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Museveni kabla ya sherehe za ufunguzi za Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) zilizofanyika Kampala, Uganda tarehe 19 Januari 2024 ………………… “Vitu lazima vitokee”, ni msemo ambao ameutumia
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba
(Mb) alipokutana na Mawaziri wenzake jijini Kampala, Uganda pembezoni mwa
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote
(NAM) na Mkutano wa Kundi la Nchi 77+China tarehe 15 hadi 22 Januari 2024. Waziri Makamba ambaye alishiriki kwa siku tatu katika
Mikutano hiyo alikutana na Mawaziri 17 kutoka nchi mbalimbali duniani kwa lengo
la kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na nchi hizo na kuweka mikakati ya
kushirikiana kiuchumi kwa manufaa ya pande zote. Waziri Makamba aliifanya Mikutano hiyo ambayo imekusanya
takriban theluthi mbili ya nchi zote duniani kama fursa muhimu ya kuitangaza
Tanzania kidiplomasia na kujadili mikakati na nyenzo za kujiletea maendeleo na
kutatua changamoto zinazoikabili dunia. Mawaziri wa Mambo ya Nje waliokutana na Mhe. Makamba
wanatoka nchi za Kenya, Msumbiji, Somalia, Malawi, Misri, Ghana, Morocco,
Filipino, Ethiopia, Singapore, Vietnam, Cuba, Iraq, Bahamas, Venezuela, Jamhuri
ya Kidemokrsia ya Congo na Azerbaijan. Masuala muhimu ambayo Waziri Makamba ameyasisitiza kwa
mawaziri wenzake ni kutumia nyezo za kawaida za kidiplomasia kukuza ushirikiano
baina ya mataifa yao. Nyenzo hizo ni pamoja na Midahalo ya Kisiasa, Tume za
Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPCs), Mikutano ya Majukwaa ya Kiuchumi, Tume
za Pamoja za Mawaziri (JMCs) na ziara za viongozi wa kitaifa. Mhe. Makamba amesema kuwa endapo vyombo hivyo
vitatumika ipasavyo vitatoa fursa kwa pande husika kukuza biashara, uwekezaji,
utalii pamoja na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa
masuala ambayo pande husika zimekubaliana. Wakati wa mazungumzo na Mawaziri wa nchi za Singapore,
Vietnam na Filipino, Mhe. Makamba alisema nchi hizo ni mfano wa kuigwa na nchi
zinazoendelea duniani kutokana na kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kipindi
kifupi. Alikubaliana na mawaziri wa nchi hizo kushirikiana
katika mafunzo, hususan, kueendeleza rasilimali watu, utalii na kilimo. Jambo lingine lililojitokeza ni ushirikiano katika
ujenzi wa miundombinu na usafiri wa anga wa moja kwa moja baina ya mataifa.
Waheshimiwa Mawaziri walijiridhisha bila shaka kuwa ukosefu wa miundombinu
unakwamisha ufanyaji wa biashara na kuongeza gharama katika uzalishaji, hivyo
wamesisitiza kutumia rasilimali za nchi zao kujiletea maendeleo. Aidha, Mhe. Waziri alisisitiza umuhimu wa kutafuta
suluhu kwa njia za kidiplomasia panapotokea migogoro ya kisiasa na
aliwahakikishia viongozi wenzake kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi
nyingine katika utatuzi wa migogoro na ujenzi wa amani duniani. Waziri Makamba katika kusimamia msemo wake wa “Vitu
lazima vitokee” alikubaliana na viongozi wenzake kufufua makubaliano ya
ushirikiano waliyojiwekea ili kuongeza kasi ya utekelezaji na kunzisha
ushirikiano rasmi na nchi ambazo Tanzania haina mikataba rasmi ya ushirikiano. | Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf. Mazungumzo hayo yalifanyika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Mchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) uliofanyika Kampala, Uganda tarehe 15 hadi 20 Januari 2024. |
|