Na Dk. Reubeni Michael Lumbagala, Kongwa.
Ni dhahiri shahiri, ajali za barabarani zimeongezeka. Kutokana na hali hii, hatua thabiti zinapaswa kuchukuliwa ili kukomesha au kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali hizo ambazo kimsingi zimekuwa zikikatisha uhai wa watu, kusababisha ulemavu wa kudumu, ongezeko la yatima, wajane na wagane.
Vilevile ajal hizo zinasababisha matumizi ya fedha katika kusafirisha na kuuguza majeruhi, fedha ambazo yamkini zingeweza kutumika katika matumizi mengine ya kimaendeleo endapo ajali hizo zisingetokea.
Agosti 30, 2022, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura akiwa Moshi mkoani Kilimanjaro wakati wa kikao kazi cha maafisa waandamizi wa jeshi la polisi makao makuu, makamanda wa polisi wa mikoa na vikosi, alisema ajali za barabarani zimeongezeka kutoka ajali 858 Juni, 2021 hadi kufikia ajali 955 Juni, 2022, ikiwa ni ongezeko la ajali 97, sawa na asilimia 11.3.
IGP Wambura amesema “Takwimu zinaonyesha kuongezeka kwa ajali 97 kutoka ajali 858 katika kipindi cha Januari hadi Juni, 2021 na kufikia ajali 955 katika kipindi cha Januri hadi Juni 2022, sawa na asilimia 11.3”. Aidha, IGP Wambura alisisitiza kuwa “Tathmini tuliyoifanya imebaini kwamba ongezeko hili limetokana na mwendo kasi na uzembe wa madereva wa vyombo vya moto, magari pamoja na bodaboda”.
Kwahiyo, kutokana na ongezeko la ajali za barabarani, madereva na watumiaji wengine wa barabara wanapaswa kuwa makini wawapo barabarani ili kuepuka ajali ambazo zinazuilika. Elimu kwa umma inayoambatana na kaulimbiu, ni muhimu kutolewa kwa wananchi wote ili kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani. Binafsi, napendekeza Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Usalama Barabarani kuja na kampeni yenye kaulimbiu: “Kawia Ufike, Jali Maisha”.
Mwendokasi umekuwa sababu kubwa ya ajali nyingi za barabarani. Baadhi ya madereva wa vyombo vya moto wamekuwa na haraka ya kufika wanapokwenda, na hivyo kuendesha kwa mwendomkali ambao mwishowake, unagharimu maisha yao, abiria na watumiaje wengine wa barabara. Wahenga walisema “Haraka haraka haina baraka”. Methali hii inasisitiza juu ya kuepuka kufanya jambo kwa haraka kwani mwisho wake unaweza usiwe mzuri.
Kampeni ya “Kawia Ufike, Jali Maisha” iweke mkazo kwa madereva kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo wa wastani ambao hata inapotokea kwa bahati mbaya kukatokea ajali, basi athari zake huwa ni ndogo, tofauti na ajali inapotokea wakati chombo kikiwa mwendokasi, ambapo watu hufariki, majeruhi kuwa wengi na uharibifu mkubwa wa vyombo vya moto. Kampeni isisitize kuwa ni bora kukawia kufika ila ufike salama, kuliko papara za kutaka kufika haraka kwa kuendesha mwendokasi ambao ni chanzo kikubwa cha ajali.
Lengo la wasafiri ni kufika salama kule waendapo bila kutokea matatizo njiani. Kampeni itilie mkazo uendeshaji wa vyombo vya moto kwa mwendo wa wastani ambao utasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani. Endapo madereva wa vyombo vya moto kama vile magari na pikipiki watazingatia kikamilifu lengo hili la safari la kufika salama, watachukua tahadhari kubwa katika uendeshaji wao kwa kuzingatia alama za barabarani.
Uhai wa watu ni jambo lenye thamani kubwa ambao kamwe haliwezi kulinganishwa na jambo jingine lolote. Madereva wanapaswa kujali maisha yao, ya abiria na watumiaji wengine wa barabara kama vile watembea kwa miguu na wasukuma mikokoteni/toroli. Njia mojawapo ya madereva kujali maisha yao ni kuepuka kuendesha vyombo vya moto kwa mwendokasi na kuzingatia sheria na alama za barabarani.
Vilevile, madereva hubeba abiria katika vyombo vyao vya moto kama vile, magari, mabasi na pikipiki. Ni vyema madereva wakathamini imani ambazo abiria wao wamewaamini kwa kupanda katika vyombo vyao vya moto. Madereva hawapaswi kuwa sababu ya abiria kujuta kupanda vyombo vyao vya moto kwa kuendesha kwa mwendokasi ambao unahatarisha maisha ya watu. Abiria waungane kwa pamoja kuwakemea madereva wanaoendesha magari kwa kasi kwa kuwashauri wapunguze mwendo na kama ushauri huo utashindwa kuzingatiwa basi wapige simu moja kwa moja jeshi la polisi kikosi cha Usalama Barabarani kwa hatua zaidi.
Wamiliki kwa vyombo vya moto kwa upande wao, wanapaswa kujali maisha yao, ya abiria na watumiaji wengine wa barabara kwa kuvitengeneza vyombo vyao mara kwa mara (service) ili kuvifanya viendelee kuwa na sifa ya kutumika barabarani. Kwa ushirikiano wa pamoja baina ya serikali, wamiliki wa vyombo vya moto, madereva, abiria na watumiaji wengine wa barabara, ajali za barabarani zitapungua kwa kiasi kikubwa. Yatosha sasa habari hizi za ajali za barabarani kila mara – Kawia Ufike, Jali Maisha.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilayani Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620-800462.