NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amechukizwa na uzembe unaofanywa na mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa madaraja katika wizara hiyo kwa kushindwa kumaliza kwa wakati na kusababisha mafuriko kwa baadhi ya maeneo.
Akizungumza wakati akikagua miundombinu ya barabara, Mhe. Shaka amesema kuwa serikali tayari imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja lakini mkandarasi huyo amekuwa akisuasua katika utekelezaji wa mradi.
Amesema kuwa makubaliano na mkandarasi huyo mpaka Januari 15, 2024 alitakiwa awe amemaliza ujenzi lakini mpaka sasa bado na kuleta usumbufu kwa wananchi.
“Mkuu wa Mkoa alipokuja mlisema mnamaliza ujenzi wa madaraja Januari 15, 2024 lakini mpaka sasa bado, niambieni tatizo ni nini? wakati pesa sio tatizo tayari mmelipwa” amesema Mhe. Shaka.
Amemtaka mkandarasi kuhakikisha anamaliza kwa wakati ujenzi wa madaraja yote katika Wilaya ya Kilosa Jambo ambalo litasaidia wananchi kupata huduma kwa wakati.