Na Mwandishi wetu, Mirerani
WACHIMBAJI wa mgodi wa Deo Minja (California Camp) uliopo kitalu B (Opec) Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamefanya misa ya kumshukuru Mungu kwenye mgodi huo unaochimbwa madini ya Tanzanite.
Lengo la misa hiyo ya madhehebu ya Katoliki (RC) ni kumshukuru Mungu kwa kufanya shughuli zao kwa usalama na amani na kumuomba Mungu aendelee kuwapa ulinzi na usalama mgodini.
Meneja wa mgodi huo, Dk Cutis Msosa akizungumza na waandishi wa habari amesema wamefanya misa ya kumshukuru Mungu kwenye mgodi huo ambao ulianzishwa zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Dkt Msosa amesema wachimbaji wa mgodi huko chini ya Mkurugenzi wake Deo Minja wamefanya misa mgodini iliyoongozwa na Padri wa Kanisa Katoliki kwa lengo la kumshukuru Mungu kwa mema yote.
“Mgodi wetu una jumuiya mbili za Wakotoliki na Walutheri hivyo huwa tunamwabudu Mungu huku tukifanya kazi kwa budii,” amesema Dkt Msosa.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wachimbaji madini ya Tanzanite kufanya kazi kisayansi huku wakimtegemea Mungu kwani migodi hiyo ipo kijiolojia.
“Tutumie njia za kisayansi huku tukiongozwa na wataalamu wa miamba (wanajiolojia) ambao Serikali imewasomesha wengi hivi sasa,” amesema.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini Mkoani Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani Rachel Njau ameupongeza uongozi wa California Camp kwa kufanya misa mgodini kwao.
“Tunapomtanguliza Mungu kwenye shughuli zetu za kila siku tunapata baraka na neema tele hivyo tunawapomgeza California Camp kwa hatua hiyo kubwa,” amesema.
Amewaasa wachimbaji wengine kuiga jambo hilo zuri kwa kufanya sala na dua kwenye migodi yao bila kujali madhehebu yao hivyo wawe wanamtanguliza Mungu.