Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dkt. Nkundwe Mwasaga (kushoto) akipokea nakala ya kitabu cha Ubunifu na Teknolojia ya Kisasa kutoka kwa mtunzi Emilian Busara leo jijini Dar es Salaam. Kitabu hicho kinachoelezea misingi ya ubunifu, biashara na teknolojia na misingi ya uongozi na ubunifu katika sekta ya teknolojia, kinalenga kuchochea kasi ya ubunifu katika teknolojia ili kuwawezesha Watanzania kuendana na kasi ya ukuaji ya Tehama duniani. (Na Mpigapicha Wetu)
……………………
Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wameshauriwa kuitumia vyema elimu ya ubunifu kiteknolojia ili kujiongezea wigo unaombatana na fursa za ukuaji wa Tehama.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk Nkundwe Mwasaga wakati alipokutana na kuzungumza na mtunzi wa vitabu, Emilian Busara aliyefika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha na kukitambulisha kitabu chake, “Ubunifu na Teknolojia ya Kisasa” kilichoandikwa katika lugha adhimu ya Kiswahili.
Dk Mwasaga alisema sekta ya Tehama inayokua kwa kasi duniani ikitumika vyema inaweza kabisa kuchangia katika ukuaji wa pato la mtu mmoja moja na taifa kwa ujumla.
“Nimefurahishwa sana na kazi yako hii. Ili sekta ikue, wapo wanaozalisha elimu na ujuzi ili viweze kuwafikia wengi. Nina imani elimu hii, tena katika lugha yetu ya Kiswahili wengi watanufaika kwa kuvuna mbinu mbalimbali za kujikita na kujiendeleza katika ubunifu,” alisema Dk Mwasaga.
Aliongeza kuwa, lengo la Tume ni kutaka kuona Watanzania wengi wanajielekeza katika ubunifu wa kiteknolojia, hasa ikizingatiwa kuwa, inalenga kuendeleza matumizi ya TEHAMA, kukuza na kuvutia uwekezaji wa TEHAMA nchini ili kutengeneza ajira na kuchangia katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
“Ubunifu kiteknolojia unalipa mno, na unatoa fursa kubwa ya ajira. Hebu chukulia mfano ya kampuni kama ya Uber na nyingine za aina hiyo. Ubunifu wao umezalisha mamilioni ya ajira katika sekta ya usafiri na usafirishaji.
“Huko ndiko dunia inakoelekea. Na katika safari hii ya ubunifu kiteknolojia, Watanzania hatupaswi kuwa nyuma. Na ndiyo maana Serikali inalenga kuanzisha vituo vya ubunifu katika sehemu mbalimbali nchini ili kuwaandaa Tanzania Kwenda sambamba na mastaifa mengine katika Uchumi wa kidigitali,” alisema Dkt. Mwasaga.
Naye Busara, msomi aliyejikita katika utafiti na uandishi wa vitabu vya fani mbalimbali, ameishukuru Tume kwa kumpokea vyema sambamba na kazi yake, akisema kitabu chake kimeegemea katika lugha ya Kiswahili akiamini kitakuwa na wasomaji wengi, hivyo kuchangia kusambaza elimu ya ubunifu kwa urahisi.
“Tumeona asilimia kubwa ya Watanzania wanazungumza Kiswahili, hivyo ili kuwafikia kwa urahisi, ni vyema tukaweka elimu yetu katika lugha yao ili kila atakayefikiwa aweze kujifunza jinsi ya kuwa mbunifu na hatimaye kuboresha wazo la kibunifu na kuwa biashara…dunia yote sasa inaelekea katika ubunifu wa kiteknolojia, ndiyo maana tunataka kushiriki katika mapinduzi haya ya kiteknolojia,” alisema Busara aliyeshirikiana Grace Mrembo kuandaa kitabu hicho.
Kitabu cha Ubunifu na Teknolojia ya Kisasa kimegawanywa katika maeneo makuu matatu yanayozungumzia Ubunifu na Teknolojia Kisasa, Biashara na Teknolojia na Uongozi na Ubunifu.