Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakili Julius Mtatiro,akizungumzia hali ya kampeni na mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu unaotajwa kutishia na kupoteza maisha ya watu wengi wilayani humo.Na Muhidin Amri
Tunduru
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro amesema,wilaya hiyo inaendelea kufanya ufuatiliaji na upimaji wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu ili kudhibiti ugonjwa huo unaotajwa kupoteza maisha ya watu wengi wilayani humo.
Amesema,serikali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kwa kushirikiana na wizara ya afya inaendelea na kampeni za uibuaji na upimaji wa maambukizi ya upimaji wa kifua kikuu kutoka kwa jamii.
“sisi eneo kubwa tunapakana na nchi jirani ya Msumbiji na tuna muingiliano mkubwa wa watu wetu na baadhi wameoleana na kuzaliana,kwa hiyo sisi kama serikali tumejipanga kuhakikisha kila mgeni anayefika lazima afuatiliwe na kupimwa afya yake kabla hajakutana na jamii zetu mkakati wa kupunguza maambukizi ya TB katika wilaya yetu”alisema Mtatiro.
Mtatiro amewataka watendaji wengine wa serikali wilayani humo,kushirikiana na wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma katika kampeni za upimaji na uibuaji wa maambukizi ya ugonjwa huo kwa kutoruhusu watu kutoka nje kuingia kiholela.
Awapongeza wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru wakiongozwa na mratibu wake Dkt Mkasange Kihongole, kwa kazi nzuri ya kufanya kampeni za uchunguzi,uibuaji na uelimishaji juu ya dalili na ugonjwa huo kwa jamii.
Kwa mujibu wa Mtatiro,kila mgeni anayefika katika wilaya hiyo kutoka nje ni lazima apimwe afya yake kama mkakati wa kuzuia maambukizi ya kifua kikuu na magonjwa mengine ya kuambukiza ili wananchi wabaki kuwa salama na kushiriki kikamilifu katika kazi za maendeleo.
Kwa upande wake mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole, ametaja makundi yaliyoko katika hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo ni wazee,watoto wadogo,wasafiri na watu wanaoishi kwenye makazi duni.
Alisema,kwa kawaida wazee ni rahisi kupata ugonjwa huo kutokana na upungufu wa kinga za mwili kwa ajili ya kukabiliana na maradhi sambamba na watoto wadogo na wale wanaoishi na magonjwa ya muda mrefu wakiwemo wanaoishi na virusi vya ukimwi.
Mkasange ametaja makundi mengine yaliyoko kwenye hatari ya kupata kifua kikuu ni wale walioko na kufanya shughuli zao kwenye misongamano, na kwenye machimbo ya madini.
Mkazi wa Tunduru Mohamed Halifa,ameshauri elimu ya kifua kikuu iendelee kutolewa kwa wananchi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini ambako hawafikiwa na huduma za uchunguzi wa ugonjwa huo mara kwa mara.
Alisema,hatua hiyo itasaidia watu wengi kufahamu dalili za ugonjwa huo,namna ya kujikinga na hatua za kufanya ili kuepuka madhara makubwa zaidi yanayoweza kutokea katika kukabiliana na ugonjwa huo unaopoteza maisha ya watu wengi wilayani humo.