Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa.
UJENZI wa nchi si kazi ndogo wala lelemala. Kuijenga nchi ni kazi ngumu inayogharimu raslimali fedha, watu, muda na mawazo bunifu.
Kwa kifupi, kujenga ni kazi ngumu kuliko kubomoa. Tangu nchi yetu ipate uhuru wake Desemba 9, 1961, juhudi kubwa inayofanyika ni ujenzi wa nchi kijamii, kiuchumi, na kisiasa.
Kwa vile Tanzania si kisiwa, ujenzi wa nchi pia unahusisha kujenga mahusiano mazuri ya nchi yetu na nchi nyingine.
Ni katika muktadha huo, Tanzania imekuwa mwanachama wa jumuiya mbalimbali za kikanda na kimataifa kwani yapo manufaa mengi kujenga mahusiano mazuri baina ya nchi yetu na jumuiya ya kimataifa.
Ujenzi wa nchi na kuifanya uhusiane vyema na jumuiya ya kimataifa si kazi ya viongozi peke yao bali ni kazi ya kila raia, yaani viongozi wetu pamoja na wananchi wote.
Kama wahenga wasemavyo “Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu” ndivyo ushirikiano wa pamoja wa viongozi na wananchi ulivyo nguzo muhimu ya kufanikisha ujenzi wa nchi yetu kwa maendeleo endelevu ya kizazi cha sasa na kijacho.
Tukiwa na sauti moja na tukiwa na nia moja, ni dhahiri kama nchi tutafanikiwa kwa haraka sana katika jitihada za kujiletea maendeleo.
Kwa mtazamo wangu, hapo nyuma, hususan kipindi baa la Uviko – 19 linasumbua dunia, uhusiano wetu na baadhi ya mataifa ya nje, ulilegalega kidogo, pengine kutokana na misimamo yetu huku wengine wakishindwa kutuelewa.
Lakini Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Dk. Samia Suluhu Hassan imekuwa na vipaumbele vingi katika kufanikisha maendeleo ya nchi na uhusiano wetu na mataifa mengine.
Moja ya kipaumbele cha Rais Samia ni kuifungua nchi kimataifa na kuhimiza diplomasia ya uchumi.
Mwanadiplomasia huyu namba moja nchini, amekuwa akihimiza nchi yetu kujenga mahusiano mazuri na mataifa mengine kwa ajili ya manufaa ya pamoja.
Mabalozi wetu wanaotuwakilisha katika nchi mbalimbali ulimwenguni wamekuwa wakihimizwa kufanya kazi kwa bidii hasa katika kutafuta fursa ambazo zitainufaisha nchi yetu ili kuchagiza gurudumu la maendeleo. Pia wanahimizwa kuvutia wawekezaji kuja Tanzania kwa wingi ili kuwekeza na hivyo kutengeneza ajira.
Kimsingi, juhudi kubwa zinafanyika kuifungua nchi yetu kimataifa kwani kufanikiwa kwa hili, kuna uhusiano wa moja kwa moja na kufanikisha mipango ya kimaendeleo kwa ustawi wa nchi na raia wake.
Ushiriki wa Tanzania katika uchaguzi wa kumtafuta Rais wa Umoja wa Mabunge Dunaini (IPU) ulikuwa ni fursa nyingine kwa nchi yetu kujitangaza kimataifa.
Katika uchaguzi huo ambao umezidi kuitambulisha Tanzania kimataifa, Spika wa Bunge letu, Dk. Tulia Ackson ndiye aliyepeperusha bendera ya nchi yetu, na Mwenyezi Mungu akawa upande wake na kushinda kwa kishindo uchaguzi huo.
Hata hivyo, kumbe mambo hayakuwa rahisi, na ugumu wa kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia kwa Dk. Tulia ukawa unawekwa na Watanzania wenyewe!
Ni vigumu kuamini kwamba wapo Watanzania walioamua kumchafua Spika wetu ili asichaguliwe kushika nafasi hiyo ambayo kwetu ni turufu muhimu kufanikisha azma ya serikali kuifungua nchi kimataifa.
Ukweli huo uliwekwa hadharani Oktoba 30, 2023, katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma kwenye hafla ya kumpongeza Dk. Tulia kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na pia kuingia kwenye rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Tulia Ackson alieleza namna alivyokutana na magumu wakati wa uchaguzi huo huku baadhi ya Watanzania wakiwa kinyume nae.
“Uchaguzi ule ulikuwa mgumu sana na hii ni kutokana na mitandao ya kijamii kutumika kunichafua. Tena waliofanya hivyo ni Watanzania wenzetu ambao walikuwa wakiungana na watu wengine ili tu nisishinde kwenye nafasi hii,” anasema Dk. Tulia.
Kiukweli inashangaza sana kuona fursa adhimu tuliyoipata tunataka kuipiga teke kwa kumchafua mgombea wetu ambaye ushindi wake unatangaza nchi yetu katika uga wa diplomasia.
Ushindi wake pia ni darasa muhimu katika kuhamasisha wasichana na wanawake kujiamini katika nyanja zote mbali na kuzidi kuitangaza nchi kimataifa.
Kasumba hii mbaya ya kuchafuana si jambo jema hasa linapokuja suala la kitaifa lenye maslahi kwa nchi yetu.
Mtu unajiuliza, hivi kumchafua Mtanzania mwenzako katika kinyang’anyiro kama hicho inakuwa inatokana na wivu, husuda, uadui au ujinga? Nimejiuliza sana.
Kuungana na adui dhidi ya ndugu yako ni kukosa uzalendo. Ni katika muktadha huo, Dk. Tulia aliendelea kusema: “Ni jambo la ajabu sana Watanzania kuungana na adui zetu kulipiga vita taifa letu. Niwaombe linapotokea suala la kitaifa tuwe kitu kimoja badala ya kuungana na adui zetu kuumizana wenyewe kwa wenyewe.”
Anasema nchi nyingi zilisema hazitaingiza wagombea ili kuipa nafasi Tanzania kuchukua kiti cha urais cha umoja wa mabunge lakini maneno ya kwenye mitandao yakawapa nguvu ya kuleta wagombea! “Lakini kwa kuwa Mungu alikuwa amepanga Tanzania ishinde hakuna kilichobadili hilo,” anasema.
Kasumba hii ya ajabu nimeiona pia katika sekta ya michezo. Inapokuja timu kutoka nje ya nchi kucheza na timu zetu, hususani zile zinazofahamika kama kubwa, baadhi ya mashabiki wa Tanzania hushabikia timu ya nje na kuacha kushabikia timu ya ndani. Wanafanya hivyo huku wakijua au kutojua kwamba matokeo yoyote mazuri ni faida kwa nchi mbali na klabu husika.
Kwa mfano, matokeo mazuri ya timu zetu katika mechi za kimataifa yamesababisha timu zetu nyingi kushiriki mashindano ya CAF na hata kama baadhi ya timu zimetolewa lakini jina la Tanzania limetajwa na timu zimepata uzoefu.
Ushindi wa timu zetu katika mechi za kimataifa, unaongeza kujiamini (confidence) na hata kuwafanya wapinzani watuogope pia tofauti na zamani walipokuwa wanatudharau sana na wanapocheza na sisi huwa na asilimia 100 ya confidence.
Bila shaka, kushabikia timu zetu hizi kubwa si uadui na hivyo tunaweza kuombeana mabaya na kukinzana tunapocheza ligi ya ndani lakini zinapokutana na timu za nje, ni vyema tuoneshe uzalendo. Kama uzalendo ukikushinda, kaa kimya na si kumshangilia au kumrahisishia mgeni amshinde mwenyeji.
Tanzania ndiyo nyumba yetu, ni vyema viongozi na wananchi kwa pamoja tuijenge nyumba yetu-Mama Tanzania, ipendeze kwenye macho ya wageni hata kama kwa ndani tuna misuguano yetu.
Linapokuja suala la kuvutia nchi yao kwenye diplomasia ya uchumi baadhi ya majirani zetu hawana utani kwa sababu wanajua hilo lina faida kwao na vizazi vijavyo. Wapo waliofikia kusema uongo kwamba Mlima Kilimanjaro hauko Tanzania bali nchini mwao!
Wakasema tena uongo kwamba hata Olduvai Gorge ambako fuvu la mtu anayesadakika kuwa wa kale zaidi duniani lilivumbuliwa, haiko Tanzania bali kwenye nchi yao!
Juzijuzi mashindano mapya ya African Football League (AFL) yalipofunguliwa Tanzania na kuvuta dunia kuja au kuiangalia Tanzania, vichwa viliwauma sana hao majirani zetu kwa mujibu wa habari za mtandao.
Kufanikiwa kwa ujenzi wa nyumba yetu kutategemea sana umoja na upendo baina yetu. Hatupaswi kugombania fito wakati tunajenga nyumba moja. Kusimama kwa nyumba yetu ni sifa yetu sote na kubomoka kwa nyumba yetu na kuonekana chafu mbele ya macho ya wageni ni fedheha kwetu sote.
Likija jingine lenye sura ya utaifa, tusirudie makosa kama anayomlalamikia Dk. Tulia. Ni kwa kudra za Mwenyezi Mungu, hili limepita salama kwamba pamoja na kuchafuliwa kwake lakini Dk. Tulia ameshinda kwa kishindo.
Tuwe wazalendo kwa nchi yetu, tuwe wamoja, tuungane pamoja kwa mambo ya kitaifa, leo yetu ndiyo kesho yetu. Tafakari, chukua hatua.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa-Dodoma. Anapatikana kwa namba: 0620 800 462.