Timu ya mpira wa miguu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje Sports Football) imeendeleza shangwe kwa mashabiki wake baada ya kuifumua timu ya mpira wa miguu ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kwa magoli 3 – 0 katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Mao Zedong’s mjini, Zanzibar.
Magoli ya Nje Sports yalifungwa na mshambuliaji Fabian David (1) katika dakika ya 35 ya kipindi cha kwanza ambalo lilidumu hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza.
Katika kipindi cha pili, Nje sports walirejea kwa kasi na kwa kupitia winga wake Yacoub Kibiga iliandika goli la pili lililopatikana dakika ya 79 na baadaye akafunga goli la tatu katika dakika ya 86 ya mchezo.
Nje Sports haikufungwa mchezo wowote tangu ilipowasili visiwani Zanzibar kwa ajili ya bonanza la michezo. Aidha, katika mechi yake ya kwanza iliyochezwa tarehe 09 Januari 2024 dhidi ya Baraza la Wawakilishi ilitoka na ushindi wa mabao (3 – 1) mechi ya pili iliyochezwa dhidi ya Ofisi ya Rais Ikulu – Zanzibar iliyochezwa tarehe 10 Januari 2024 ilitoka na ushindi mnono wa magoli (8 – 3) na katika mechi yake ya leo dhidi ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imeibuka na ushindi wa goli 3 – 0.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ameipongeza Nje Sports kwa ushindi mnono na kuzitaka timu zote mbili kuendeleza michezo kwa kuwa michezo ni afya na inaimarisha ushirikiano baina ya wachezaji na jamii.
Naye Kocha wa Nje Sports, Bw. Shaban Maganga amesema pamoja na ushindi walioupata wataendelea kujifua zaidi na kuhakikisha kuwa kikosi chake kinakuwa imara wakati wote.