Na Sophia Kingimali
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amezielekeza hospitali zote za serikali kuhakikisha zinaweka dawati la huduma kwa wateja ili kusaidia kupokea malalamiko ya wagonjwa na kuyatafutia ufumbuzi.
Maelekezo hayo ameyatoa leo Jumatano 11, 2024 jijini Dar es salaam wakati wa kikao chake na waandishi wa habari akielezea hali ya utoaji huduma za afya kwa mwaka 2023 na mikakati yake kwa 2024.
Amesema kumekua na mafanikio mengi katika utoaji wa huduma za afya lakini pia kumekua na changamoto nyingi ambazo zinatafutiwa ufumbuzi ikiwemo upungufu wa watumishi na mwitikio mdogo wa wananchi kujiunga na mifuko ya huduma za afya kwani ni asilimia 15 tu ya wananchi wenye bima hizo.
“Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwani imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya mafanikio tunayoyaona leo ni kazi kubwa ya Rais wetu ili kuhakikisha kila mwananchi anakua na afya njema”amesema Ummy.
Amesema changamoto nyingine ambayo imekua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya utoaji huduma za afya ni usimamizi usioridhisha kwa baadhi ya watumishi.
Akizungumzia mikakati ya mwaka 2024 Ummy amesema wizara imejipanga kuimarisha afua za kinga ili kuwezesha wananchi kujikinga na magonjwa lakini pia kuwezesha ufumbuzi wa mapema kwa magonjwa.
“Tutaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza ikiwemo kuhimiza kufanya mazoezi na kuzingatia ulaji kwani asilimia kubwa ya magonjwa yanasababishwa na mfumo wa maisha”amesema.
Sambamba na hayo amesema ili kuboresha huduma ya tiba utalii hospitali za serikali zinapaswa kushirikia na taasisi binafsi kuhakisha wanatoa huduma kwa wagonjwa wanaotoka nje ikiwemo marazi,chakula na huduma nyingine ili kuendelea kuvutia zaidi wagonjwa kutoka nje kuja kutibiwa nchini.
“Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuboresha huduma za kibobezi imeweza kuvutia wagonjwa mbalimbali kuja kupata huduma na takwimu zinaonyesha mwaka 2022 wagonjwa kutoka nje walikua 1,699 lakini 2023 idadi imeongezeka na kufikia 1,937″amesema.
Amesema Tanzania imekua kimbilio la wagonjwa wengi kutoka nje ya nchi na wagonjwa hao wanaleta fedha za kigeni na kuchangia kwenye pato la Taifa.