Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa
………………………..
Na Sophia Kingimali
MAMLAKIA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) imetaja mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2023 na kuainisha mikakati saba wanayotarajia kuitekeleza mwaka huu ukiwemo wa kuanza kwa matumizi ya bandari ya Kavu ya Kwala.
Akizungumza jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Januari 9,2024 Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa amesema mamlaka hiyo ina jumla ya bandari kubwa sita ikiwa tatu za mwambao wa bahari(Dar es Salaam, Mtwara naTanga) na tatu zikiwa maziwa makuu yaani ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Mbossa amesema kwa kipindi cha Julai hadi Desemba , mwaka jana, TPA ilijiwekea lengo la kuhudumia meli 792 na hadi kufikia Desemba, mwaka jana ilikuwa imevuka lengo na kuhudumia meli 979 sawa na asilimia 123.6.
“Kwa upande wa ukubwa wa meli zilizohudumiwa, TPA ilikuwa na lengo la kuhudumia meli zenye ukubwa wa tani 15,576,000 katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka 2023 ambapo hadi kufikia mwezi Desemba, 2023, TPA
ilikuwa tayari imehudumia meli zenye ukubwa wa kiasi cha tani 17,200,692 sawa na asilimia 110.4,” amesema
Amesema TPA ilikuwa na lengo la kuhudumia kiasi cha tani 10,993,000 katika bandari ya Dar es Salaam na hadi kufikia Desemba, mwaka jana ilihudumia tani 12,052,682 sawa na asilimia 109.6 za lengo.
Akizungumzia maboresho ya bandari amesema TPA imeendelea kutekeleza jukumu la kuhudumia meli na shehena ambapo kati ya mwaka wa fedha 2023/2024 kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya meli na shehena katika bandari ya Dar es Salaam.
Amesema ongezeko hilo ni matokeo ya mikakati ya maboresho ya huduma za bandari ikiwa ni pamoja na kufanya kampeni za kimasoko na kuonana ana kwa ana na wateja wa ndani na nje ya nchi.
Pia kuboresha huduma kwa wateja, kutoa tozo shindani, kuimarisha ofisi za kimasoko zilizopo nje ya nchi na kufungua mpya, ushirikiano na wateja na wadau wa bandari na kusomana kwa mifumo.
Aidha Mbossa amesema TPA imeamua kutenganisha utekelezaji wa mradi wa bandari ya Bagamoyo na mradi wa eneo maalumu la kiuchumi Bagamoyo.
Awali ilielezwa ujenzi wa mradi wa bandari ya Bagamoyo utahusisha ujenzi wa eneo maalumu la kiuchumi.
“Tunaanzia na gati mbili ndefu na hizo zitajengwa na sisi TPA tupo tayari kupokea mwekezaji kutoka sekta binafsi atakayeijenga bandari hiyo kushirikiana na serikali,” amesema.
Mkurugenzi huyo alitaja changamoto zinazoikabili bandari hiyo kuwa ni uchache wa magati, miundombinu isiyotosheleza ya reli na barabara ambayo ingerahisisha uondoshaji wa shehena bandarini kwa haraka.
Changamoto nyingine ni kuharibika mara kwa mara kwa midaki, mitambo ya kuhudumia shehena, ongezeko kubwa la meli kulinganisha na uwezo wa bandari, utoaji wa huduma kusimamishwa na mvua za El-Nino, baadhi ya gati kutumika katika shughuli za kijamii na uchimbaji wa gati namba nane hadi 10.