Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava akizungumza wakati Kamati yake ilipotembelea kazi ya Uboreshaji Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi inayofanywa na timu ya wataalamu mkoani Arusha tarehe 8 Januari 2023.
Mbunge wa Viti Maalum CCM Lucy Mayenge akichangia hoja wakati Kamati ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii ilipotembelea na kupata taarifa ya kazi ya Uboreshaji Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi inayofanywa na timu ya wataalamu mkoani Arusha tarehe 8 Januari 2023.
Mbunge Festo Sanga akichangia hoja wakati Kamati ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii ilipotembelea kazi na kupata taarifa ya Uboreshaji Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi inayofanywa na timu ya wataalamu mkoani Arusha tarehe 8 Januari 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipokwenda jijini Arusha kukagua kazi ya Uboreshaji Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi tarehe 8 Januari 2024.
Baadhi ya wataalamu wanaofanya kazi ya kufanya Maboresho Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi.
………..
Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kufanya Kazi kubwa na nzuri ya Maboresho ya Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi inayofanywa na timu ya wataalamu mkoani Arusha.
Akizungumza mara baada ya hitimisho la wasilisho la kazi ya uboreshaji mfumo huo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Timotheo Mzava ameipongeza Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa na nzuri na kueleza kuwa kazi hiyo inakwenda kuacha alama kwa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha uongozi kwa kuiacha sekta ya ardhi katika mifumo bora.
” Nichukue fursa hii kumpongeza Mhe Rais kwa kazi hii nzuri, kama kamati wameridhishwa na kazi na hongereni sana na mfumo huu uende ukawe bora na kutoa huduma kwa watanzania” alisema Mhe Mzava.
Baadhi ya wabunge wamesema mfumo huo siyo tu utarahisisha na kuharakisha huduma za sekta ya ardhi bali utajibu maswali mengi yakiwemo ya kijamii.
“Niipongeze wizara ya ardhi kwa kufanyia kazi mfumo utakaojibu maswali mengi ya kijamii na ningetamani mfumo huu ungejibu maswali na changamoto za kiuchumi” alisema Mhe. Lucy Mayenga mbunge wa viti Maalum.
Mbunge Makete mkoani Njombe Festo Sanga aliipongeza Wizara kwa kuboresha mfumo na kueleza kuwa uboreshaji huo umechelewa ingawa uko katika hatua nzuri. Hata hivyo, mbunge huyo wa Makete alitaka kufahamu utayari wa wizara ya Ardhi katika kutumia mfumo hususan kwenye eneo la usalama wa mifumo.
Aidha, Mbunge wa jimbo la Tabora Mjini Emanuel Adamson mbali na kuipongeza wizara kwa kuboresha mfumo alitaka kufahamu uimara wa utekelezaji mfumo huo kwa kuwa kumekuwa na mifumo mingi lakini wakati wa utekekezaji kumekuwa na changamoto ikiwemo kuekezwa mtandao uko chini.
Mfumo huo unganishi wa usimamizi wa sekta ya ardhi unatarajiwa kuanza katika mikoa mitano ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Tanga na utarahisisha na kuharakisha upatikanaji huduma za sekta ya ardhi kwa kuwa wananchi watakuwa wakipata huduma kwa njia ya mtandao.