……………..
Makumbusho ya Taifa la Tanzania imeingia Mkataba wa miaka mitano na Chuo Cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kilichopo Mbegani wilayani Bagamoyo kushirikiana kwenye sekta ya Uhifadhi wa viumbe wa majini kwa kufanya utafiti na mafunzo yatakayowawezesha wataalamu wa Taasisi hizo kubadilishana uzoefu wa namna ya utendaji kazi kwenye uhifadhi na uvuvi wa kitalii(sports fishing)
Akizungumza baada ya zoezi la kusaini mkataba lililofanyika Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt.Noel Lwoga amesema uwepo wa mkataba huu ni mwanzo wa kuimarisha utafiti na programu za elimu katika historia na urithi wa majini ikiwemo teknolojia na uvuvi wa asili na kisasa utakaoendana na uhifadhi na maonesho ya mila na utamaduni katika nyumba za asili za Kituo cha Kijiji cha Makumbusho, ambacho hivi karibuni kimeboreshwa kwa kujenga nyumba za asili kwa mfumo wa kaya kwendana na ramani ya Tanzania na ujenzi wa mfano wa Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu FETA, Dkt.Semvua Mzighani amesema ushirikiano huu ni wa manufaa makubwa kwao kwa kuwa watapata fursa nzuri ya kujifunza namna bora ya uhifadhi wa masalia ya viumbe wa majini na kwamba chuo chao kiko tayari kuleta wataalamu wa kufundisha uvuvi wenye tija na uvuvi wa kitalii lakini pia kujikita kwenye Tafiti na mafunzo hususan katika aina mbalimbali za samaki na viumbe wa majini ambao wako hatarini kutoweka.