Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
KATIBU Mkuu Kiongozi , Balozi Dkt .Moses Kusiluka amewahakikishia wawekezaji nchini kwamba Serikali inaendelea kuwaunga mkono na kuwawekea mazingira rafiki na wezeshi kutekeleza majukumu yao kirahisi.
Aidha Serikali itakaa chini na Wataalamu na Makatibu wakuu wa sekta zinazogusa shughuli za uwekezaji kuangalia namna ya kutatua changamoto inayowakabili ya upungufu wa nishati hasa gesi.
Vilevile ,Kusiluka amewaasa watendaji wa Wilaya na Mikoa kujenga tabia ya kukutana na wawekezaji ili kujua changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi.
Hayo aliyasema katika ziara yake ya kutembelea viwanda viwili vya nguo na vipodozi vilivyojengwa ndani ya Kongani ya SINO TAN ,Kwala wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani, huku akiwa ameambatana na Waziri wa fedha Mwigulu Nchemba ,Waziri wa Viwanda na Biashara na makatibu wakuu wa wizara ya Uchukuzi,Fedha,Viwanda na Biashara na Taasisi wezeshi.
Alieleza Serikali ya awamu ya sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji, na Tanzania ni eneo salama kwa uwekezaji.
“Kwa muda mfupi tumeona matokeo ya malengo yenu, na tunaendelea kuwapa uhakika kuwa tunalipa umuhimu wa juu sana kongani hii” alieleza Kusiluka.
Kusiluka alifafanua ,leo hii tunashuuhudia uwekezaji huo mkubwa wa awali, kongani itakuwa na viwanda zaidi ya 200 ikiwemo vya nguo, Tanzania ina zalisha pamba lakini asilimia 80 inauzwa nje ya nchi.
“Kwa ujenzi huu ,na kiwanda hiki cha nguo itakuwa ni sehemu nzuri ya kuuza pamba yetu ndani ya nchi” alieleza.
Awali mratibu wa mradi wa kongani ya Sinotan Jensen Hung alisema, kongani ya Sinotan itakamilika 2027 ,wanatarajia kujenga viwanda vya kati na vikubwa 300 na kutoa ajira za moja kwa moja 100,000, sanjali na kuchangia pato kwa mwaka trilioni 1.3.
Alitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa nishati ya umeme na gesi.
Pia kukosa miundombinu rafiki, ushindani wa uwekezaji ambapo anasema kuanza kwa SGR na Bandari Kavu Kwala kutasaidia kuvutia wawekezaji zaidi katika kongani hiyo.
Waziri wa viwanda na Biashara ,Dkt. Ashatu Kijaji alieleza, kama wizara wanatamani kuona kongani hiyo inajaa viwanda.
Aliwapongeza Sinotan kwa kuanza utekelezaji haraka na sasa kufikia ujenzi wa viwanda viwili ambapo wametoa ajira hivyo vikikamilika viwanda vyote 300 ongezeko la ajira litakuwa kubwa .
Waziri wa fedha Mwigulu Nchemba, alieleza Katibu Mkuu kiongozi ametoa muongozo, wizara ya fedha ni wadau wa kila uzalishaji,hivyo wanaunga mkono juhudi za ujenzi wa kongani hiyo.
Aliwahakikishia wawekezaji hao huo mradi ni wa mfano ,watashughulikia changamoto zinazogusa wizara hiyo ikiwemo masuala ya kodi.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, alhaj Abubakari Kunenge alieleza viwanda vingi vinasuasua kutokana na u pungufu wa nishati ya umeme na gesi.
Hata hivyo, mkoa umejipanga vizuri katika suala la uwekezaji na ujenzi wa viwanda.