Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kukamilika kiwanda cha kusarifu Mwani Chamanangwe kitakuwa na uwezo wa kununua tani 30,000 za Mwani kwa wakulima.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipoweka Jiwe la Msingi Kiwanda cha kusarifu Mwani Chamanangwe Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba tarehe 05 Januari 2024.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa kiwanda hicho kitapokamilika ajira zitapatikana, bei itapanda pamoja na soko la uhakika la nje kutokana na kusarifu hapa nchini.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuwawezesha Wakulima wa Mwani kwa kuwapatia maboti , mashine pamoja na zana mbalimbali za kuzalisha Mwani ili kuongeza uzalishaji kwa wingi wa Mwani.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa kujengwa kiwanda hicho ambacho ni kikubwa Afrika inatokana pia kuwa Zanzibar ni nchi inayoongoza kwa kuzalisha zao hilo Afrika.
Vilevile amesema kuwa Mikoa ya Tanzania Bara ya mwambao ikiwemo Mtwara, Tanga wako tayari kuuza Mwani Zanzibar.