Mbunge wa Singida mjini ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano Mazingira), Musa Sima.
Na Dotto Mwaibale, Singida.
MBUNGE wa Singida mjini ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano Mazingira), Musa Sima ametoa photokopi mashine sita kwa ajili ya kurahisisha kazi katika shule za msingi na sekondari mkoani Singida.
Akizungumza juzi katika hafla ya kukabidhi photokopi mashine moja kwa Shule ya Sekondari ya Mufumbu iliyopo Kata ya Kisaki mkoani hapa alisema lengo lake ni kuhakikisha walau kila shule zilizopo katika jimbo lake la uchaguzi zinapata mashine hizo.
“Changamoto kubwa iliyopo katika shule zetu ni kupata huduma ya photokopi mashine kwani wanalazimika kwenda mjini au kwa watu binafsi jambo ambalo linawapotezea muda na ndio maana nimeguswa kusaidia katika eneo hilo” alisema Sima.
Alisema mpaka sasa amekwisha toa photokopi nne katika shule za sekondari na moja katika shule ya msingi na nyingine kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Singida.
Katika hatua nyingine Sima amemshukuru Rais Dkt.John Magufuli kwa kuwapatia vifaa vya maabara ambapo Shule ya Sekondari ya Mufumbu imekuwa ya kwanza kupata vifaa hivyo.
Alisema katika kumuunga mkono Rais Dkt.John Magufuli katika sekta ya afya na elimu ametoa mifuko ya saruji 300 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Kisaki.
Sima aliongeza kuwa katika sekta ya elimu amemsaidia kumsomesha mwanafunzi aliyefanya vizuri mwaka 2018 katika mtihani wake kwa Kanda ya Kati aliyetoka Shule ya Sekondari ya Mufumbu aliyepata Divisheni 1.8 ambaye kwa sasa anaendelea na masomo shule ya Ilboru.
Mbunge Sima alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kujenga tabia ya kusaidia shughuli za maendeleo badala ya kuiachia serikali pekee.