Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa taarifa ya tathmini ya hali ya joto na mwenendo wake katika maeneo mbalimbali nchini.
Ongezeko la joto nchini husababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua unaojitokeza katika maeneo mbalimbali. Kwa kawaida vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).
Aidha, wastani wa ongezeko la joto la dunia katika mwaka wa 2023 ulifikia nyuzi joto 1.40C na ulivunja rekodi na kuwa ni mwaka wenye joto zaidi katika historia ya dunia, ukichagizwa na uwepo wa El Niño na mabadiliko ya tabianchi. Kwa upande wa Tanzania, tathmini zinaonesha pia wastani wa ongezeko la joto kwa mwaka 2023 ulikuwa nyuzi joto 1.00C kwa upande wa Tanzania na pia kuufanya mwaka 2023 kuvunja rekodi na kuwa mwaka wenye joto zaidi katika historia.
Katika kipindi cha mwezi Disemba, 2023 kumekuwepo na ongezeko la joto kwa baadhi ya maeneo nchini hususan nyakati ambazo kumekuwa na vipindi vichache vya mvua. Hadi kufikia tarehe 29 Disemba, 2023 kituo cha Morogoro kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto 33.9 °C ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 1.3 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Disemba. Kituo cha Tanga kiliripoti nyuzi joto 33.6 °C mnamo tarehe 01 Disemba (ongezeko la nyuzi joto 1.5), Dodoma nyuzi joto 33.5 °C mnamo tarehe 19 Disemba (ongezeko la nyuzi joto 2.9), Dar es Salaam nyuzi joto 33.2 °C mnamo tarehe 02 Disemba (ongezeko la nyuzi joto 1.2) na Zanzibar nyuzi joto 33.4 °C mnamo tarehe 02 Disemba, 2023 (ongezeko la nyuzi joto 1.6).
Hata hivyo, katika kipindi cha mwezi Januari, 2024 vipindi vya mvua vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika maeneo mengi nchini. Hali hii inatarajiwa kusababisha kupungua kwa joto katika baadhi ya maeneo hususan yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.