Tanzania Assemblies of God (TAG) Mwenge Christian Center ( MCC) kupitia hafla ya mkesha wa mwaka mpya 2024 imetoa Tuzo ya Heshima kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila kutambua mchango wake katika kutunza na kuendeleza maadili ya kitanzania hususani katika Mkoa huo.
Akiongea wakati anakabidhi Tuzo hiyo kwa muwakilishi wa Mkuu Mkoa wakati wa mkesha huo Mhe Diwani wa Kata ya Kijitonyama Mhe Dama Samora, Mchungaji kiongozi wa kanisa hilo Mch Abdiel Meshack Mhini amesema amekua akifuatilia namna Mkuu wa Mkoa anvyokemea kwa vitendo tabia ovu zinazofanyika katika jamii zetu ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya, biashara za ngono kupitia madangulo ambapo Mkuu wa Mkoa amekua akipita yeye mwenyewe kubomoa madangulo ” vitendo hivyo vya kutunza na kuendeleza maadili ya kitanzania ambayo mkuu wa Mkoa amekuwa akifanya TAG Mwenge tumeona tumtie moyo kwa kumpatia Tuzo hii” Alisema Mch Abdiel Mhini.
Aidha Mch Abdiel Meshack Mhini katika risala yake amesema Kanisa limekuwa likishirikiana na Serikali inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau wengine katika kuijenga jamii ya kitanzania inayoheshimu katiba na sheria za nchi kujenga na kulinda maadili mema na kuwafanya wengi kuwa wacha Mungu.
Vilevile Mch Abdiel amesema Kanisa linapitia Changamoto mbalimbali wakati wa kutoa huduma za kiroho ambazo amiomba Serikali kuzipatia ufumbuzi kama vile kukatika kwa umeme mara kwa mara, miundombinu ya barabara kufika kanisani hapo ni mibovu, pia urasimu wa kutoa vibali katika ofisi za Serikali pale ambapo kanisa linahitaji kibali fulani
Kwa upande wa muwakilishi wa Mkuu wa Mkoa Mhe Dama Samora amewapongeza kwa maandalizi mazuri ya mkesha huo, na kuwataka kuondoa shaka katika changamoto wanazopitia ambapo amewahakikishia kumfikishia mkuu wa Mkoa risala waliyoisoma kama ilivyo kwa utekelezaji.
Ifahamike kuwa Kanisa la TAG Mwenge liliandaa mkesha maalum kwa kuabudu na kuomba kwa ajili ya mtu mmojammoja, jamii na Taifa kwa Ujumla ikiwa ni ishara ya kuaga mwaka 2023 na kukaribisha mwaka mpya 2024.