Mgeni rasmi wa half ya chakula cha watoto yatima, Mkuu wa Idara ya Falsafa na Maadili,Chuo Kikuu cha Mtakafifu Agostino (SAUT) Mwanza,Padri Dr.Innocent Sanga(wa nne kutoka kulia),leo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wageni waalikwa, kutoka kushoto wa tano ni Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke.
Sheikhe wa Shia Ithna Asheri Kanda ya Ziwa,Hashimu Ramadhani akizungumza kabla ya hafla ya chakula cha yatima leo jijini Mwanza amesema watoto wanapochezea mavumbi wanatukumbusha tumetokana na udongo ambako tutarudi na siku moja Mungu atatutoa kwa mujibu wa Mtume S.A.W.
Mkurugenzi wa Shirika la Kuvulini, Yasin Ally akizungumza leo wakati wa hafla ya chakula cha yatima jijini Mwanza kuwa Watanzania warudi katika utamaduni wa kuwalea yatima akitolea mfano mwenye mali akifa wanaye hugombaniwa tofauti na maskini kisa mali alizoacha.
Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke,akizungumzia umuhimu wa jamii kuwalea yatima wakati wa hafla ya chakula cha yatima kilichoandaliwa na The Rocky Solution leo.
Mgeni rasmi katika hafla ya chakula cha yatima kilichoandaliwa na BAKWATA kwa hisani ya The Rocky Solution akizungumza katika hafla hiyo leo jijini Mwanza.
Ofisa Uhusiano wa Jamii wa Kampuni ya The Rocky Solution Ltd,Diana Magesa, akitoa nasaha zake kabla ya chakula cha watoto yatima kilichoandaliwa na kampuni ikishirikiana na BAKWATA Mwanza.
Mgeni rasmi wa hafla ya chakula cha yatima,Padri Dr.Innocent Sanga (kulia), leo akimkabidhi cheti Diana Magesa kwa niaba ya Mkurugenzi wa The Rocky Solution Ltd,Zakaria Nzuki,cheti hicho kimetolea na BAKWATA kwa kutambua mchango wake.
Watoto yatima wa vituo mbalimbali jijini Mwanza leo wakijumuika kula chakula na viongozi mbalimbali pamoja na mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Falsafa na Maadili-SAUT Mwanza,Padri Dr. Innocent Sanga (kushoto).
Baadhi ya viongozi wadini ya Kiislamu wakishiriki kula chakula na yatima leo jijini Mwanza kusherehea Mwaka Mpya.

……….

NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA

MASHIRIKA baadhi Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) na vituo vya kulelea watoto yatima yanadaiwa kujinufaisha kwa fedha za misaada inayotolewa na wahisani kusaidia watoto hao.

Madai hayo yametolewa leo na Mkuu wa Idara ya Falsafa na Maadili,Chuo Kikuu cha Mtakafifu Agostino (SAUT) Mwanza,Padri Dr.Innocent Sanga,wakati wa chakula na yatima kilichoandaliwa na BAKWATA mkoani humu ilishirikiana na  Rocky Solution Ltd.

Akizungumza kabla ya chakula hicho Padri Dr.Sanga amesema baadhi ya NGO’s na vituo vya kulelea yatima vinawatumia watoto hao kibiashara na kujinufaisha kwa fedha za misaada inayotolewa na wahisani.

Amesema serikali katika kukomesha tabia hiyo itunge sera ya kuvipata vituo vya kuwalea,kuwatetea na kuwalinda yatima pamoja na kutengeneza mifumo ya kuwabaini katika vitongoji,vijiji na mitaa.

“Tahadhari,serikali yawezekana inaogopa, baadhi ya NGO’s na vituo vya watoto yatima,vinawatumia kibiashara na kujinufaisha,wanawafanya kama bidhaa na wanakula fedha zao baada ya kuandika maandiko ya kuomba fedha kwa wahisani,”amesema Padri Dr.Sanga.

Ameishauri serikali kuhakikisha vituo na mashirika hayo yanasajiliwa,ifanye uratibu na ufuatiliaji kwa wanaojinufaisha kwa fedha za yatima na kuwachukulia hatua za kisheria.

“Tumewakandamiza yatima kwa njia mbalimbali,Tanzania imegeuka janga kubwa la yatima kudhulumiwa,kuonewa na kunyang’anywa mali zao na ndugu,hivyo tutafakari dhambi hii na kutubu,”amesema Padri Dr.Sanga.

Mkuu huyo wa Idara ya Falsafa na Maadili ya chuo cha SAUT Mwanza,pia ameishauri serikali itenge bajeti ya kuwasaidia yatima kupata elimu na miongoni mwao wana uwezo mkubwa kiakili.

Pia amesema changamoto ya watoto yatima kukimbilia mitaani ni matunda ya kutukanwa na kukandamizwa na ndugu zao ili kuwaepuka maadui hao wanaowakamindamiza wakihofia usalama wao.

Aidha Padri Dr.Sanga amesema mila za kigeni zimeharibu upendo kwani mila za kiafrika kukaa na yatima ni kawaida na  kumhudumia kama familia ni utamaduni wetu,hivyo huwezi kumwacha akakimbilia mtaani kwani dini zetu zinashughulika na mema kwa matendo na si maneno.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Wakili Kiomoni Kibamba,katika chakula hicho amesema hatua kujiona tuko katika dunia ya ustaarabu kumesababisha kuacha misingi kwa kukosa ucha Mungu.

“Zamani miji yote haikuwa na watoto wa mitaani,tujiulize wametoka wapi? Tunazidi kuharibikiwa na kuiharibu jamii,bila kujali imani tumebaki na majina ya dini na kukosa ucha Mungu,tumekuwa dhulumati  na roho mbaya,”amesema.

Wakili Kibamba amesema hakuna mcha Mungu ataadhirika na anayetaka kufanikiwa amchukue yatima na kumlea kwani hakutaka kufiwa na wazazi na Mungu alivyo fundi kifo hakichagui cheo, kabila, rangi wala kabila ya mtu.

Awali Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikh Hasani Kabeke amesema anatamani kuona kila Mtanzania akimchukua yatima na kuishi naye na kutoa wito kwa waliojaliwa kuwa na uwezo kiuchumi wavisaidie vituo vinavyowalea yatima.

“Mtume Muhammad S.A.W.anasema atakayekaa na yatima na kumtendea vizuri atakuwa naye bega kwa bega,natamani kila Mtanzania amchukue yatima na kumtendea wema ili kumuondolea huzuni aliyo nayo,”amesema na kuongeza, chakula hicho cha yatima huandaliwa kila mwaka na kampuni ya The Rocky Solution kwa miaka sita sasa.