Usemi usemao hakuna marefu yasiyokuwa na ncha umetimia leo ambapo jumla ya maafisa na Askari 29 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) wamehitimu mafunzo ya mabadiliko ya kimuundo leo tarehe 20 Juni, 2026 katika Kituo cha Mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi kilichopo Mlele mkoani Katavi.
Akifunga mafunzo hayo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TAWA Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko amewataka wahitimu kuzingatia taratibu na sheria na amri zote za Jeshi la Uhifadhi
“Mmepata mafunzo ya kubadilika kimuundo kutoka raia kuwa Jeshi, matumaini yangu ni kuwa kila mmoja wetu hapa mtabadilika na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa katika kusimamia uhifadhi na rasilimali za nchi”,alisema Meja Jenerali (Mst) Semfuko.
Mkuu wa wilaya ya Mlele Mhe. Majid Mwanga amewapongeza wahitimu hao na kuwataka kuwa mfano mwema wa uzalendo, maadili na ujasiri katika utendaji kazi.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Abdul-Razaq Badru amewahimiza wahitimu hao kutumia mafunzo waliyoyapata kuimarisha uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.
Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mlage Kabange amesema ushirikiano uliooneshwa kati ya TAWA na Ngorongoro katika kusimamia mafunzo hayo unaonesha kuimarika kwa Jeshi la Uhifadhi nchini na ari ya kusimamia rasilimali za Wanyamapori na Misitu.
Akitoa taarifa kuhusu mafunzo hayo mkuu wa mafunzo Meja Breyman Rulenguka amesema Jumla wa watumishi 29 wamefaulu na kupata alama za kuridhisha ambapo mwanafunzi mmoja pekee hakuweza kuhitimu kutokana na sababu za kiafya.
Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa katika kituo hicho kwa lengo la kuimarisha Jeshi la Uhifadhi na utendaji kazi wake.

