Mhandisi wa maji kutoka ofisi ya Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira manispaa ya Songea(Souwasa) Charles Kitavile kulia na baadhi ya watumishi wa Souwasa wakikagua shughuli za uchimbaji wa mtaro wa maji katika kata ya Subira.
Mkazi wa kata ya Subira katika manispaa ya Songea ambaye hakutaka kutaja jina lake,akivuta maji kutoka kwenye kisima kwa ajili ya matumizi,hata hivyo serikali kupitia mamlaka ya maji na usafi wa mazingira manispaa ya Songea SOUWASA imenza kutekeleza mradi wa maji ya bomba utakaogharimu zaidi ya Sh.bilioni 1
……..
Na Mwandishi Wetu, Songea
SERIKALI,imetenga Sh.bilioni 1.168 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji ya bomba utakaowaondolea adha ya huduma ya maji safi na salama wakazi zaidi ya 12,000 wa kata ya Subira katika manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Hayo yamesemwa na Mhandisi wa maji kutoka ofisi ya meneja wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira manispaa ya Songea(Souwasa) Charles Kitavile.
Kitavile ametaja kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa nyumba mbili za kuhifadhi mashine(pump house) tenki la kuhifadhi maji lita 200,000 na kupeleka umeme kwenye mashine za kusukuma maji.
Kazi nyingine ni kuchimba mitaro na kulaza mabomba umbali wa kilomita 45.5 na hadi sasa kazi zilizofanyika ni ununuzi wa mabomba,kuchimba mitaro urefu wa kilomita 14.5 na utekelezaji wake umefikia asilia 25.
Kitavile amewataka wananchi ,kuhakikisha wanatunza miundombinu ya mradi huo ili uweze kudumu kwa muda mrefu na usaidie kumaliza changamoto ya huduma ya katika maeneo yao.
Baadhi ya wakazi wa kata hiyo,wameiomba serikali kukamilisha ujenzi wa mradi huo haraka ili waweze kuondokana na gharama kubwa wanayopata ya kununua ndoo moja ya lita 20 kwa Sh.1,000.
Wamesema,wananchi wasiokuwa na uwezo wa fedha wanatumia maji ya visima vya asili ambayo siyo safi na salama na hivyo kuhatarisha afya zao kwa kupatwa na magonjwa ya mlipuko yanayotokea mara kwa mara.
Hamis Hassan alisema,katika mtaa wao kwa muda mrefu wanatumia maji ya mito yaliyochanganyika na uchafu unaotoka milimani na visima ambavyo maji yake siyo safi na salama kwa kuwa visima hivyo vimezungukwa na makazi ya watu.
Alisema,wanaotaabika kwa kiasi kikubwa ni wanawake na watoto ambao ndiyo watumia wakubwa wa maji kwa kufua nguo na kupikia ambapo mtoto hawezi kwenda shuleni akiwa mchafu wa mwili na sare za shule.
“katika kijiji chetu maji ni shida kubwa,tunaona mradi umeanza kutekelezwa lakini kama ujenzi wake unakwenda kwa kusua sua,tunaiomba serikali kukamilisha ujenzi wake haraka ili uweze kutunusuru na gharama kubwa ya kununua ndoo moja ya maji kwa Sh.1,000 na wakati mwingine kwenda hadi kata jirani ya Majengo kuchota maji”alisema.
Halima Mbaraka alisema, katika kata ya Subira maji ya bomba ni changamoto kubwa na ya muda mrefu na wananchi wasio na kipato hulazimika kutembea umbali mrefu kufuata maji kata za jirani.
Alisema, kwa sasa wanategemea visima kupata maji kwa ajili ya matumizi yao,hata hivyo wakati wa kiangazi vinakauka kutokana na ukame na kutegemea visima vilivyochimbwa kwa mikono.
Lucia Komba,amefurahishwa na hatua ya serikali kupitia mamlaka ya maji na usafi wa mazingira manispaa ya Songea(Souwasa)kwa kuanza kutekeleza mradi huo wa maji ya bomba.
Amewaomba wasimamizi wa mradi huo(Souwasa),kufikisha mtandao wa mabomba kwenye maeneo mengine ambayo yanakabiliwa na kero kubwa ya huduma ya maji ili wananchi waweze kufaidi matunda ya serikali yao ya awamu ya sita.