Na Muhidin Amri,
Songea
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas,amewataka wakazi wa mkoa huo kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo waliyojiwekea kwa mwaka mpya 2024,badala ya kutumia muda wao kukaa vijiweni.
Alisema,serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri na rafiki kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kufanya shughuli zao za maendeleo na kupata huduma bora za kijamii, hivyo wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo kwa kufanya kazi kwa bidii na siyo kupiga soga vijiweni.
Kanal Laban ametoa wito huo jana,wakati akitoa salamu za mwaka mpya 2024 kwa wananchi wa mkoa huo kupitia vyombo mbalimbali vya Habari katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa mkoa mjini Songea.
Alisema,ni muhimu kwa kila mmoja atumie muda wa mwisho na mwanzo wa mwaka kutafakari namna ya kupigania maendeleo yake,familia,mkoa na Taifa kwa ujumla kwa kuenzi shughuli zilizompatia mafanikio kwa mwaka uliopita 2023 na kuweka mikakati nini cha kufanya kwa mwaka mpya 2024.
Mkuu wa mkoa,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia wakulima wa mkoa huo ruzuku ya mbolea iliyowezesha wakulima na mkoa kupata mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo.
Kanal Laban alisema,pamoja na kuwa katika sherehe za mwisho na mwanzo wa mwaka ni muhimu kuendelea na shughuli zao za kilimo kwa kutenga fedha kwa ajili ya kununua pembejeo za ili waendelee kufanya vizuri katika kilimo.
Kanal Laban ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Ruvuma,amewakumbusha wazazi na walezi kuhakikisha wanafanya maandalizi ya watoto wao kwenda shule kwa kununua vifaa na mahitaji yote muhimu kabla shule hazijafunguliwa wiki ijayo.
Aidha,amempongeza Rais Samia, kwa kuupatia mkoa huo fedha nyingi zilizotumika katika ujenzi wa miundombinu ya elimu, afya,barabara, kiwanja cha ndege,sekta ya uvuvi,meli kupitia ziwa Nyasa na bodi za kisasa.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa ni kwamba, uwezeshaji huo umeufanya mkoa wa Ruvuma kuwa katika sura mpya ya maendeleo katika kipindi kifupi cha miaka miwili ya uongozi wake.
Katika hatua nyingine mkuu wa mkoa,amewataka wananchi kufuata na kutii sheria ikiwemo kuacha vitendo vya kujinyonga ambayo vinaacha majonzi kwa familia na kupoteza nguvu kazi ya mkoa huo na Taifa kwa ujumla na kwamba,sababu kubwa ya kushamiri kwa matukio hayo ni wivu wa kimapenzi
Alisema,kwa sasa mbolea inauzwa kwa bei ndogo kati ya Sh.55,000 hadi 65,000 ambayo imeshawishi wananchi wengi kujikita na shughuli za kilimo na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara katika mkoa huo.
Aziz Halfan,ameiomba serikali kupitia wakala wa barabara za mjini na vijijini(Tarura)kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ya pembezoni ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao.
Alisema, sehemu kubwa ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma wanategemea kilimo katika maisha yao,kwahiyo kama serikali itaboresha barabara zake itakuwa rahisi kwa wakulima kupeleka mazao yao moja kwa moja sokoni.
Badala ya wanunuzi kutumia ubovu wa barabara kwenda moja kwa moja shambani kununua mazao kwa bei ndogo isiyolingana na uzalishaji mashambani.
