Ndugu Wananchi, Leo, tarehe 31 Disemba, tunauaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024.
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia neema ya uhai na afya njema. Wapo ndugu zetu na jamaa zetu ambao tungependa kuwa nao leo hii ila Mungu amewapenda zaidi.
Tuendelee kumuomba awapumzishe pema peponi. Nasi tulio hai tuombe tujaaliwe Siha, Nguvu na furaha, tushushiwe Neema na Baraka, tujaaliwe Hekima na Busara katika kuendesha mambo yetu.
Ndugu wananchi, Mwaka 2023 ni mwaka uliokuwa na neema, lakini pia uliokuwa na changamoto zake kwetu kama nchi. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuumaliza mwaka tukiwa na umoja na mshikamano.
Hotuba yangu ya leo itajikita katika mapito ya mwaka huu na matarajio yetu kwa mwaka ujao. MAFANIKIO NA CHANGAMOTO ZA MWAKA 2023Amani, ulinzi na usalama Ndugu Wananchi, Nikianza na suala la Amani, Ulinzi na Usalama wa nchi yetu, ninafarijika kusema kwamba, mipaka yote ya nchi yetu iko salama.
Aidha, vikosi vyetu vya ulinzi na usalama vipo imara. Sote tulishuhudia namna vikosi vyetu vilivyojitoa katika uokoaji na kurejesha hali ya kawaida pale tulipopatwa na maafa.
Nitumie fursa hii kuvipongeza kwa ujasiri na uzalendo wao. Aidha, nawashukuru na kuwapongeza wananchi kwa kuendelea kudumisha amani na umoja wa kitaifa. Mapito ya Kiuchumi Ndugu Wananchi, Tukiangalia mapito ya Kiuchumi, tunaona kwamba pamoja na athari za janga la UVIKO-19, kwa sasa dunia pia inakabiliwa na athari za vita zilizosababisha uchumi wa kidunia kudorora, hususan kwenye sekta muhimu za uzalishaji.
Hali hii imeongeza gharama na mfumuko wa bei kwa bidhaa za msingi kama vile chakula na mafuta ya vyombo vya usafiri na mitambo, hali ambayo, kwa ujumla imevuruga mnyororo wa ugavi wa kimataifa.
Riba kwenye masoko ya fedha imepanda, upatikanaji wa Dola za Marekani pia umeathiriwa. Katika kuuhami uchumi wetu, tulitekeleza sera madhubuti za fedha ili kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa bei, kuchochea ukuaji na kuimarisha udhibiti katika sekta hiyo ya fedha. Tumeendelea kudhibiti mfumuko wa bei, ambao katika kipindi cha Januari hadi Novemba, 2023 ulipungua hadi wastani wa 3.9%, ikilinganishwa na wastani wa 4.3% kipindi kama hicho mwaka jana.
Aidha, ukuaji wa Uchumi na Pato la Taifa kwa mwaka 2023 ulikadiriwa kuongezeka kwa 5.2% ikilinganishwa na 4.7% mwaka jana wa 2022. Katika mwaka 2022/23, Serikali ilifanikiwa kupokea kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.3 sawa na Shilingi Trilioni 3 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, sawa na 100% ya kiasi kilichopangwa kukopwa.
Hata hivyo, deni la Taifa limeendelea kuwa himilivu. Uwiano wake kwa pato la Taifa, kwa thamani ya sasa, ni 35.6% ukilinganisha na ukomo wa 50%.
Kutokana na utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara nchini (Blueprint) na sera zinazolenga kuifungua nchi, tumeweka mazingira rafiki ya kibiashara, na Mwaka huu, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilisajili miradi 504 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.6, ikiwa ni ongezeko la 58% ikilinganishwa na miradi 292 iliyosajiliwa mwaka 2022. Kati ya miradi iliyosajiliwa, miradi 55 ilikuwa ni ya upanuzi, hali inayoashiria imani kubwa ya wawekezaji kwenye uchumi wetu na mwenendo wa ukuaji wake.
Mwaka huu pia tulifanikisha tathmini ya hadhi yetu kwenye ukopeshwaji iliyofanywa na kampuni za Moody’s na Fitch, hatua ambayo itazidi kujenga imani Kimataifa na kuvutia mitaji ya wawekezaji mbalimbali hapa nchini kwetu.
Kwa upande wa ukusanyaji wa kodi, kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 2023 ukusanyaji ulifika shilingi trilioni 22.6, ikiwa ni ongezeko la 8% ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2022. Hivyo, jinsi uchumi wetu unavyokua, tutaendelea kuongeza makusanyo kupitia mifumo madhubuti ya ukusanyaji na kuhakikisha kodi inakusanywa kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria.
Ndugu wananchi, Sekta za uzalishaji, zinazojumuisha Kilimo (kilimo, ufugaji na uvuvi), Madini na Utalii, ndio tegemeo la uchumi na hivyo tumeendelea kuweka msisitizo kwenye sekta hizo, ili kuwafikia wazalishaji wengi zaidi, hususan wale wadogo na kuchochea uzalishaji kuanzia ngazi za chini. Waswahili husema, utajiri hupatikana ardhini.
Kwa muktadha huo, tumeongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 751 mwaka jana 2022 hadi shilingi bilioni 970 mwaka huu, sawa na ongezeko la 29%. Shabaha yetu ni kuchochea kiwango cha ukuaji wa sekta ya kilimo kufikia 10% kwa mwaka, ifikapo mwaka 2030.
Uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 17,148,290 (milioni kumi na saba laki moja elfu arobaini na nane mia mbili na tisini) msimu wa 2021/2022 hadi tani 20,402,014 (milioni ishirini laki nne na elfu mbili na kumi na nne) msimu wa mwaka 2022/2023, hivyo kufikisha 124% ya kiwango cha utoshelevu wa chakula nchini.
Aidha, Serikali imetoa shilingi bilioni 116 kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) ili kuchochea soko, ambapo katika awamu ya kwanza, NFRA imenunua jumla ya tani 200,293 (laki mbili mia mbili na tisini na tatu) za mazao.
Vilevile, tumehakikisha mazao makuu yanauzwa kwa njia ya minada ili kupata bei nzuri, na tumeanzisha mnada mpya wa zao la chai. Hadi Novemba 2023, tani 204,818.16 (lakini mbili elfu nne mia nane na kumi na nane nukta moja sita) za mbolea zilikuwa zimesambazwa kwa wakulima katika Mikoa yote ya Tanzania Bara, ikiwemo ruzuku ya Serikali yenye thamani ya shilingi bilioni 67.82.
Serikali inaendelea kutoa ruzuku ya mbolea, mbegu na viuatilifu kwa baadhi ya mazao ya kimkakati kama vile pamba, korosho, alizeti, chikichi, kahawa na chai. Vilevile, Serikali imeendelea na jitihada za kuwaingiza vijana na wanawake kwenye uzalishaji.
Mpaka tunamaliza mwaka huu 2023, jumla ya ekari 201,241. (laki mbili elfu moja mia mbili arobaini na moja nukta sita) zimetengwa kwa shughuli hiyo. Aidha, tumeanzisha programu ya kilimo cha kisasa iitwayo Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ili kuongeza uzalishaji, kuchochea viwanda vya usindikaji, na kutengeneza ajira kwa vijana.
Kwa upande mwingine, Serikali itaendelea kuwekeza kwenye skimu za umwagiliaji ili kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 727,000 (laki saba elfu ishirini na saba) hadi hekta 822,000 (laki nane na elfu ishirini na mbili) ifikapo Disemba 2024Tumeendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya madini, ambapo mwaka huu tumeshuhudia ongezeko la 6.43% la thamani ya madini yaliyozalishwa.
Pia, kumekuwa na ongezeko la 5.8% ya madini yaliyouzwa nje ya nchi hadi kufikia dola za Marekani bilioni 3.15. Kwa kutambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo kwenye sekta hii, mwaka huu, Serikali ilinunua mitambo mitano (5) ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji hao ili kuongeza tija zaidi na mchango wao kwenye sekta ya madini.
Mwelekeo wa Serikali ni ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini hapa nchini, hatua itakayotuwezesha kuongeza thamani na fursa zaidi za ajira.
Utalii Kwenye sekta ya utalii, kwa kipindi cha Oktoba mwaka jana hadi Oktoba 2023, tumepokea watalii 1,750,557 (milioni moja laki saba na elfu hamsini mia tano hamsini na saba), ikilinganishwa na watalii 1,381,881 (milioni moja laki tatu elfu themanini na moja na mia nane themanini na moja) walioingia kipindi kama hicho mwaka 2022. Katika kipindi hichohicho, mapato kupitia sekta ya utalii yalifikia Dola za Kimarekani Bilioni 3.22 ikilinganishwa na Dola za Kimarekani Bilioni 2.33 kipindi kama hicho mwaka 2022.
Manufaa haya yametokana na juhudi za Serikali na wadau wa sekta hii. Hivyo, nitoe rai kwa watoa huduma kwenye sekta ya utalii, kuendelea kuimarisha huduma zao, na kwa Watanzania wanaoishi maeneo ya vivutio, tuendelee kudumisha ukarimu kwa wageni ili tuendelee kupokea watalii wengi zaidi. Ndugu wananchi, Uzalishaji na ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa unachochewa na miundombinu ya usafiri na mawasiliano.
UchukuziKwa upande wa usafiri wa nchi kavu, mwaka huu, Serikali imeendelea kukamilisha na kuanza ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko katika Mikoa mbalimbali.
Serikali pia iliendelea na utekelezaji wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambapo vipande vya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Makutupora vimefikia zaidi ya 90%.
Aidha, tumepata udhamini wa Benki ya Maendeleo Afrika utakaowezesha uendelezaji wa kipande cha Tabora-Kigoma na Uvinza-Musongati.
Nimekuwa nikisikia mabadiliko ya tarehe za kuanza kwa safari za treni, na kwa kweli, wananchi wamechoshwa na vijisababu, wanataka kuona reli ikifanya kazi. Sasa, naelekeza, ifikapo mwisho wa mwezi Julai 2024, safari kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma zianze.
Kwenye usafiri wa majini, tumekamilisha ujenzi wa gati katika bandari mpya ya Karema kwenye Ziwa Tanganyika. Bandari hii itafungua uchumi, biashara, na muingiliano wa watu na DRC na hivyo kukuza uchumi wa Mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi. Vilevile, tumekamilisha ujenzi wa gati, ghala, jengo la abiria, ofisi na sehemu ya kuegesha meli katika Bandari ya Ndumbi, katika Ziwa Nyasa.
Kwa upande wa usafiri wa anga, Serikali ilikamilisha ununuzi wa ndege moja ya mizigo na moja ya abiria. Aidha, mashirika mbalimbali ya ndege ya Kimataifa kama vile Air France na Saudi Airlines, yalivutiwa kuanza kutoa huduma za safari kuja nchini. Tunaamini uwekezaji huu utaimarisha sekta ya utalii na utakuza pia biashara ya kilimo cha maua na mbogamboga.
Nishati Ndugu wananchi, Kuhusu sekta ya nishati, kwa kipindi cha takriban miezi minne ya mwaka huu wa 2023, nchi yetu imekumbwa na upungufu wa umeme, uliosababisha mgao.
Ukweli ni kwamba, kwa muda mrefu suala la mgao wa umeme nchini limekuwa likijirudia. Ni kwa msingi huo basi, mwaka 2017, Serikali ilifanya uamuzi wa kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo hili kwa kutekeleza mradi mkubwa wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, ambao utakapokamilika utaongeza Megawati 2,115 kwenye Gridi ya Taifa. Habari njema ni kwamba, panapo majaliwa, mwezi Februari 2024 tutawasha rasmi mtambo wa kwanza na mwezi Machi tutawasha mtambo wa pili.
Mitambo hii miwili itatupatia jumla ya Megawati 470 na hivyo kufidia upungufu wa sasa ambao ni Megawati 300 tu. Hatua hii itakwenda sambamba na kuwasha mtambo wa Rusumo utakaoongeza Megawati 27.
Ni imani yangu na Serikali kwa ujumla kuwa, hatua hizi zitaleta ufumbuzi wa kudumu kwa suala la mgao wa umeme nchini.
Aidha, Serikali inaendelea kuwekeza kwenye vyanzo vingine vya umeme kama vile gesi, jua, na upepo, ili kuongeza uhakika wa umeme.
Nikizungumzia umeme vijijini hadi kufikia mwezi Novemba, 2023 Serikali ilikuwa imepeleka umeme katika vijiji 11,447 (elfu kumi na moja mia nne na arobaini na saba) sawa na 93% ya vijiji vyote 12,318 (elfu kumi na mbili mia tatu na kumi na nane) vya Tanzania Bara. Kazi ya usambazaji wa umeme vitongojini nayo inaendelea.
Ndugu Wananchi, tunapoimarisha sekta za uzalishaji na ukuaji wa uchumi, linalenga kuimarisha ustawi wa watu. AfyaNguvu kubwa iliwekwa kwenye kuimarisha huduma za afya nchini kwa kuajiri wataalam, ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendea kazi.
Mwaka huu 2023 , Serikali imeajiri jumla ya wataalam 17,309 (elfu kumi na saba mia tatu na tisa) na ilitenga jumla ya shilingi bilioni 190.9 kwa ajili ya kununua dawa.
Kwa upande wa vifaa tiba, tumeweka MRI 5 na CT – Scan 30 kati ya 32 katika vituo vya kutolea huduma katika Mikoa 24 kati ya 26. Tumesambaza seti 123 za vifaa vya huduma kwa watoto wachanga na wenye uzito pungufu, na mashine 125 za mionzi yaani ultra sound.
Vilevile, tumetoa mashine 140 za kutibu dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama. Aidha, tumesambaza magari 369 ya kubebea wagonjwa na uratibu wa huduma za afya kote nchini.
Nirejee wito wangu kwa Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Wilaya na Mikoa tulikopeleka vifaa hivi, wavitunze na unapotokea uharibifu, ukarabati ufanywe na wataalam, ili viendelee kutusaidia.
Pale tulipopeleka fedha za majengo hakikisheni majengo yanajengwa kwa ubora unaotakiwa na vifaa husika vinawekwa kwa wakati.
Ndugu wananchi, Uwekezaji tunaoufanya kwenye sekta hii unaleta matokeo. Kwa mfano, kuanzia mwezi Januari mpaka Novemba, 2023, jumla ya wananchi 15,386 wamepata huduma za CT – Scan kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini kote na hii imesaidia katika kuimarisha mfumo wa rufaa na huduma za uchunguzi kwa Mikoa yote.
Jumla ya Wagonjwa 200 wamepimwa kipimo cha MRI katika Hospitali za Rufaa za kanda ya Mbeya, Chato, na Mtwara. Hospitali hizi hazikuwahi kuwa na kipimo cha aina hii, hivyo uwepo wa mashine za MRI zimeleta ahueni ya gharama kwa Wananchi wa kanda husika.
Kwa upande wa Matibabu ya Kuchuja Damu kwa Wagonjwa Sugu wa Figo yaani Dialysis, Hospital 11 za Rufaa za Mikoa zinatoa huduma kwa wagonjwa 438. Kabla ya hapo wagonjwa hao wangelazimika kufuata huduma hii kwenye ngazi za juu (Kanda, Maalum na Taifa) na hivyo kuongeza gharama za matibabu zisizokuwa za moja kwa moja.Serikali itaendelea na uwekezaji wa huduma za Afya za Kibingwa ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za aina yeyote kulingana na uhitaji wake.
Maji Kwenye sekta ya maji, tuliendelea kufanya uwekezaji mkubwa uliotuwezesha kukamilisha miradi 506 ikiwemo 436 ya vijijini na 70 ya mijini yenye uwezo wa kuhudumia wananchi 5,754,340 (milioni tano laki saba na elfu hamsini na nne mia tatu arobaini). Hivyo, tumeongeza wastani wa upatikanaji wa huduma za maji hadi 88% mijini na 77% vijijini.
Aidha, tumepata dola za Marekani milioni 600 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Dodoma. Kwa wananchi, tukumbuke kwamba kila tone la maji lina gharama, ni wajibu wetu kulipia maji jinsi tunavyotumia.
Kwa watendaji wa sekta, hakikisheni mnaendelea kutoa elimu kwa jamii na kuchukua hatua stahiki ili kulinda vyanzo vya maji.
ElimuNikiangalia sekta ya elimu, pamoja na uendelezaji wa miundombinu ya shule zetu, mwaka huu pia Serikali iliboresha Sera na Mitaala ya Elimu. Lengo ni kuhakikisha elimu yetu inatoa ujuzi muafaka kwa watoto wetu kuweza kujiajiri, na wale watakaoingia kwenye soko la ajira, basi wakidhi mahitaji ya soko hilo kwa mazingira ya ulimwengu wa sasa. Aidha, inafahamika kwamba walimu wetu bado wana changamoto ya makazi.
Hivyo, tutafanya jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba kuanzia mwaka ujao wa fedha, tunajielekeza kwenye kuboresha maslahi ya walimu ikiwemo ujenzi wa nyumba za kuishi.
Kwa upande wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, bajeti imeongezeka kutoka shilingi bilioni 654 mwaka wa fedha uliopita hadi shilingi bilioni 731 mwaka huu.
Aidha, idadi ya wanufaika imeongezeka kutoka 198,105 (laki moja elfu tisini na nane mia moja na tano) mwaka uliopita hadi 220,075 (laki mbili elfu ishirini na sabini na tano) mwaka huu, ambapo wanafunzi 73,513 (elfu sabini na tatu mia tano na kumi na tatu) ni wanufaika wa mwaka wa kwanza.
Vilevile, mwaka huu, Serikali imetenga bajeti ya shilingi bilioni 48 kwa ajili ya kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi 8,000 wa stashahada (diploma) kwa fani za kipaumbele.
Wito wangu kwa wote waliokwishafaidika na mikopo ya elimu ya juu, wahakikishe wanarejesha mikopo yao kwa wakati ili iweze kuwanufaisha na wengine. Kwa upande mwingine, ili kuhamasisha wanafunzi kupenda na kujiunga na masomo ya sayansi, mwaka jana Serikali ilianzisha fursa za ufadhili wa masomo au maarufu kama Samia Scholarship.
Ufadhili huu unaozingatia uwezo na ufaulu wa wanufaika. Mwaka 2022, kiasi cha Shilingi Bilioni 2.94 kilitumika kuwafadhili wanafunzi 636 kwenye masomo ya sayansi katika vyuo mbalimbali.
Mwaka huu, Serikali imetenga Shilingi Bilioni 6.7 ambayo hadi sasa inawafadhili wanafunzi 1,019. Nitoe rai kwa wanufaika kutumia fursa hii vizuri na kusoma kwa bidii. Ushirikiano wa Kimataifa Ndugu wananchi,Kwenye medani za Kimataifa tumeendelea kung’ara.
Nyote ni mashuhuda wa namna tulivyoshiriki mikutano mbalimbali yenye ushawishi na mvuto kiuchumi kama Mikutano ya BRICS, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Jukwaa la Uchumi la Davos na pia mikutano ya Afrika na nchi mbali mbali zenye nguvu za kiuchumi. Vilevile tumepokea wageni wakubwa na mashuhuri kutoka Mataifa ya Marekani, Ujerumani, Indonesia, Hungary, na Romania pamoja na nchi jirani na rafiki za Afrika.
Kutokana na kuimarika kwa ushirikiano wetu na Mataifa na mashirika mbalimbali, kupitia ziara nilizofanya mwaka huu, baadhi ya mafanikio tuliyopata ni kama ifuatavyo:- Tumepata kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 550 kwa ajili ya miradi ya usalama wa chakula; Tumepata Dola za Marekani milioni 297.64 kwa ajili ya mradi wa mawasiliano vijijini; Chuo cha Teknolojia cha IIT Madras kutoka India ambacho kimefungua Kampasi Zanzibar; Tumepata soko la mabondo ya samaki, parachichi, kahawa, soya na kadhalika; Tumepata nafasi za kazi 500 kwa wauguzi wetu kutoka nchini Saudi Arabia n.k; Baada ya takribani miaka sita, tumerejeshwa kwenye Mfumo wa Changamoto za Milenia (MCC) wa Marekani, ambapo utekelezaji utaanza mwakani. Kutokana na mwenendo wetu mzuri kwenye uchumi, mwezi huu tumepokea kutoka Benki ya Dunia dola za Kimarekani milioni 500 kwa ajili ya kusaidia bajeti ya Serikali.
Ninaitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi wanaotuwakilisha nje ya nchi, kuwa wabunifu zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kubainisha fursa katika nyanja za Kimataifa na kuzileta nyumbani.
Aidha, kwa upande wa Wizara zinazonufaika na miradi na fursa kutoka nje, zihakikishe zinatumia fursa hizo kwa wakati na kutekeleza miradi kwa muda unaokubaliwa.
Mazingira na Mabadiliko ya Tabia Nchi Ndugu WananchiMwaka huu, nchi yetu ilikabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mvua za El Nino zilileta uharibifu wa miundombinu, na kuongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko na malaria.
Hivyo, tunapoanza mwaka mpya, nazitaka Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuchukua tahadhari kuzuia mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza pamoja na malaria.
Aidha, kila Halmashauri iendelee kupanda na kutunza miti milioni 1.5 kila mwaka, kama ilani ya CCM inavyoelekeza.
Ndugu wananchi, Ninayo furaha kuwaeleza kuwa katika Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi mwaka huu (COP28), Tanzania iliahidiwa na Jumuiya ya Kimataifa chini ya Uongozi wa Global Centre on Adaptation na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 9.9 kwa ajili ya miradi itakayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Aidha, katika Mkutano wa nane wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (Global Environment Fund – GEF) jumla ya dola milioni 53 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya mazingira na maendeleo Tanzania. Vilevile, katika kupambana na uharibifu wa mazingira nchini, mwaka huu, nilizindua Programu ya matumizi ya nishati safi inayolenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa Barani Afrika. Mwakani 2024 tutaiwekea programu hii, mfumo rasmi wa kuifanya iwe endelevu na yenye manufaa. Programu hiyo itatusaidia pia kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wenye lengo la kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.
Ni vizuri tukaanza kujielekeza kwenye matumizi ya nishati safi, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa sana kwa uchumi wetu.
Sekta ya Michezo Ndugu Wananchi,Kwenye sekta ya michezo, pamoja na kuimarisha miundombinu ikiwemo ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa, mwaka huu tumepata mafanikio mengi ya kujivunia ikiwemo yafuatayo:- Timu ya Taifa ya Tanzania kufuzu mashindano ya CHAN mwaka 2024; Tanzania kufanikiwa kushinda fursa ya kuwa moja ya waandaaji wa mashidano ya AFCON mwaka 2027; Timu ya Zanzibar Chini ya umri wa Miaka 15 (Karume Boys) kutwaa ubingwa wa mashindano ya CECAFA chini ya umri wa miaka 15; Timu ya mpira wa miguu ya JKT Queens kuwa bingwa wa mashindano ya CECAFA mwaka 2023; Tanzania kuwa mwenyeji wa michuano ya kwanza ya African Super League, huku Timu ya Simba ikiwa ya kwanza katika ukanda wa CECAFA kushiriki mashindano hayo; Timu ya Yanga kupata medali ya mshindi wa pili kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF Confederations Cup); na Binti wa kitanzania, Magdalena Shauri, kuwa mshindi wa tatu kwenye mbio za Berlin Marathon na mwanariadha Alphonce Simbu kuwa mshindi wa pili kwenye mbio za Shanghai Marathon.
Natumia fursa hii kuzipongeza timu zote zilizofanya vyema na wanamichezo wote waliofanya vizuri mwaka huu. Ahadi yetu ni kuendelea kuwekeza kwenye michezo hususan kwa vijana, kwani michezo ni ajira pia.
Hivyo, tutahakikisha tunaendelea kulea vipaji kuanzia ngazi za shule kwa kuhakikisha michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA inaendela kufanyika. UTEKELEZAJI WA FALSAFA YA ‘R’ NNE (4R’s) Ndugu Wananchi, Mwaka 2023, tuliongeza kasi ya utekelezaji wa falsafa ya R nne (4R’s), ambayo inazungumzia maridhiano, mageuzi, ustahimilivu na kujenga upya.
Kwa upande wa mageuzi (reforms), tulichukua hatua zifuatazo kuimarisha ufanisi na utendaji kazi: Tuliunda Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Tulitenganisha Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi; tuliunda Wizara mpya ya Mipango na Uwekezaji; na tuliongeza Naibu Waziri na Katibu Mkuu wenye dhamana na Jumuiya ya Afrika Mashariki; Tulirejesha Tume ya Mipango, ili iratibu utekelezaji wa mipango yetu na kuandaa Dira mpya ya maendeleo; Tuliunda Tume ya Kuboresha Masuala ya Haki Jinai na Tume ya kutathmini Ufanisi na Utendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Utekelezaji wa mapendekezo ya kiutendaji ya Tume hizo yanaendelea na mwakani tutaendelea kufanyia kazi mapendekezo yanayohitaji mabadiliko ya sera na sheria; Tulianza marekebisho kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kuimarisha usimamizi wa Mashirika ya Umma. Sambamba na hilo, katika kuongeza ufanisi na tija, mwaka huu, tumeunganisha Mashirika ya Umma na taasisi 16, na kufuta Mashirika manne (4); Mwisho, tuliingia ubia na sekta binafsi kwa ajili ya ukodishaji na uendeshaji wa sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam gati Na. 4-7 kwa lengo la kuongeza ufanisi wa huduma kwenye bandari hiyo.
Ndugu Wananchi, Katika kutekeleza falsafa ya maridhiano, tuliendelea na utekelezaji wa maazimio yaliyotokana na majadiliano na wadau wa demokrasia nchini.
Ili kutekeleza maazimio hayo, tayari tumewasilisha Bungeni Miswada mitatu kuhusu Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Sheria ya Vyama vya Siasa. Niwashukuru wadau wa siasa kwa kuweka maslahi ya nchi mbele na niwaahidi kwamba, tutaendelea kushirikiana nao. Kwa upande mwingine, tumeendelea kushuhudia vyama vyote vya kisiasa vikitekeleza shughuli zao kwa uhuru na uwazi kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
MWELEKEO WA MWAKA 2024 Ndugu wananchi,Baada ya mapito hayo ya mwaka unaoisha leo na kubainisha baadhi ya mafanikio tuliyopata, nitumie fursa hii kuainisha kwa kifupi masuala machache tunayoyatarajia mwakani. Mwakani tunaadhimisha miaka 60 ya Muungano na miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Matukio haya muhimu kwa Taifa letu ni chachu ya kuendelea kudumisha umoja wa Kitaifa na kuimarisha ustawi wa jamii yetu; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni tukio jingine tunalolitarajia mwakani kwa tarehe itakayotangazwa na Mamlaka husika.
Nitoe rai kwa Watanzania kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo, ili tuchague viongozi wanaotufaa; Mwakani pia, tutaendelea kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuhakikisha usalama wa chakula.
Tutaendelea kutekeleza programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT). Aidha, tutaanza kutekeleza miradi ya kuuza na kukodisha kwa bei ya ruzuku zana za kilimo kwa wakulima ikiwamo matrekta; Vile vile tutaendelea pia na mageuzi (reforms) katika sekta mbalimbali, ikiwemo uendeshaji wa mashirika ya umma na taasisi, lengo likiwa kuongeza ufanisi na tija katika uendeshaji wake. Tutaimarisha pia utekelezaji wa Sera ya Elimu ili kuhakikisha kuwa tunaanda watoto wetu kwa mazingira ya sasa.
Vilevile, tutaendelea na mchakato wa kuandika Dira Mpya ya Maendeleo; Mwakani pia, kwa mujibu wa sheria tutaboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Natoa wito kwa wote wenye sifa wajitokeze pindi zoezi hilo litakapotangazwa na Mamlaka husika; Umuhimu wa Kampuni Changa, yaani StartUps, umeendelea kukua nchini. Serikali itaendelea kushirikiana zaidi na taasisi tanzu za Kampuni Changa, na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ustawi wake.
Pamoja na mikutano mingine, tutakuwa wenyeji wa Kilele cha Nchi 25 za Afrika zinazozalisha Kahawa. Katika kuendelea kujenga uhimilivu na uwezo wetu wa kukabiliana na majanga, ikiwemo majanga ya moto, Serikali itachukua hatua za kulijengea uwezo zaidi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na taasisi nyingine zinazoshirikiana nazo ili kujenga uwezo wa kukabiliana na majanga ikiwemo majanga ya moto.
Kwa upande wa michezo tutakuwa wenyeji wenza wa michuano ya kombe la Afrika kwa wachezaji wa ndani yani CHAN. Hii ni fursa kubwa ya kibiashara tuichangamkie. Ndugu wananchi, ni sahihi kusema kwamba, mwaka 2023 ulikuwa ni mwaka wa mageuzi na mwaka ujao 2024 utakuwa ni mwaka wa utekelezaji na matokeo zaidi. Natoa rai kwa wananchi wenzangu, kuazimia kubadilika, kila shughuli halali tunayoifanya tuifanye kwa bidii, maarifa na uadilifu na InshaAllah, Mwenyezi Mungu atabariki kazi za mikono yetu. Kwa upande wa Serikali, tutaendelea kusimamia haki, uadilifu, uwajibikaji na nidhamu ya utendaji serikalini.
HITIMISHO Ndugu Wananchi, Kama ilivyo ada, nitumie fursa ya mwisho wa mwaka huu kutoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri kutimiza wajibu wao na kuchukua tahadhari ili kuepusha ajali zitokanazo na uzembe.
Vilevile, kwa kutambua kwamba msimu wa mvua unaendelea na madhara yanaweza kujitokeza kwa baadhi ya maeneo ya nchi yetu, hatuna budi kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia maelekezo ya Mamlaka husika.
Nihitimishe kwa kuwashukuru sana kwa imani na ushirikiano mkubwa mlioutoa kwa Serikali na kutuwezesha kutekeleza vyema majukumu yetu kwa mwaka 2023.
Na namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kheri na fanaka katika mwaka mpya 2024, uwe ni mwaka wa mafanikio zaidi, na tuendelee kufanya kazi kwa weledi, bidii, maarifa na uadilifu, ili kazi iendelee.
Mungu ibariki Afrika,Mungu ibariki Tanzania, AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA!