Mwonekano wa baadhi ya madarasa ya awali
……
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Ikiwa imebaki takriban wiki moja ili kuanza kwa muhula mpya wa masomo kwa shule za msingi na sekondari hapo Januari 8 mwaka 2024; mkoa wa Katavi unatarajia kuchukua jumla ya wanafunzi 42,974 wa darasa la awali na wanafunzi 39,326 wa darasa la kwanza.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari Mkuu wa Mkoa wa Katavi Bi. Mwanamvua Mrindoko amesema kwa kipindi cha Januari hadi Disemba 2023 mkoa huo ulipokea kiasi cha shilingi bilioni 19.4 kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika shule za msingi na sekondari.
Mkuu huyo wa mkoa wa Katavi aliongeza kuwa katika fedha hizo wameweza kujenga shule mpya kumi za msingi na kuongeza vyumba vya madarasa katika baadhi ya shule.
Aliongeza kuwa madarasa hayo yataweza kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuwapokea wanafunzi wapya wa madarasa ya awali na darasa la kwanza.
Aidha Bi. Mrindoko amewaagiza wazazi wenye watoto wa kuanzia umri wa chini ya miaka mitano kuhakikisha wanawaandikisha watoto shule.‘Kwa wazazi au walezi watakaokiuka agizo hili tutawachukulia hatua kwani sheria zipo’ alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Elimu mkoa wa Katavi, Mratibu wa Elimu mkoa bwana George Mtawa amesema lengo ni kuandikisha wanafunzi 42,974 wa darasa la awali na mpaka sasa wameandikisha wanafunzi 15,189 sawa na asilimia 35.34%.
Kwa upande wa darasa la kwanza amesema lengo ni kuandikisha wanafunzi 39,326 na wameandikisha wanafunzi 23,051 sawa na asilimia 58.62%.Pia ametoa wito kwa wazazi na walezi wawaandikishe watoto shule.
Amesema serikali imekwishajipanga kuwapokea wanafunzi wapya, hivyo ni wajibu wa wazazi kuhakikisha wanakamilisha mahitaji ya muhimu ikiwemo sare za shule na madaftari.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi ambao hawajawaandikisha watoto shule (majina tunayahifadhi) waliofikiwa na mwandishi wetu wamekuwa na sababu kadhaa ikiwemo kukosa fedha za sare na wengine wakidai hawana vyeti vya kuzaliwa vya watoto.
‘Mimi sijampeleka mtoto nasubiri baba yake atoke shamba ndio tukamwandikishe maana nikienda mwenyewe watasema ni mtoto wa mzazi mmoja’ alisema mama mmoja mkazi wa Mpanda.
Aidha kwa wazazi waliowaandikisha watoto kuingia madarasa ya awali wengi wao wamefurahia ubora wa miundombinu iliyojengwa na serikali na hata kufikia kufananisha madarasa yake na yale yanayopatikaana katika shule za binafsi za kulipia.
Kwa upande wa walimu wakuu wa shule tofauti za msingi; walipoulizwa kuhusu wanafunzi kuhudhuria na nguo za nyumbani wako waliokubali watoto wafike bila hata ya sare za shule na wako waliopinga.
‘Wewe fikiria ndugu mwandishi serikali imejenga madarasa mazuri kama haya ya awali halafu wewe ulete mtoto wako hapa amevaa yebo! Wawanulie viatu’ alisema mwalimu mkuu mwingine
.‘Inapendeza mtoto akija shule awe amekamilika, na hata akipita njiani anafahamika ni mwanafunzi, lakini kutokana na hali zetu kutofautiana inabidi kuwaruhusu hata wasio na sare kuja shule watanunua polepole’ alisema mwalimu mwingine.