Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamsaka Dereva aliyekuwa akiendesha Gari lenye namba za usajili T.428 DXD/T.860 BWM aina ya FAW mali ya kampuni ya Cedars Investment Limited ya Jijini Dar es Salaam anayefahamika kwa majina ya Msafiri Mohamed @ Mwawila ambaye amekimbia muda mfupi baada ya kusababisha ajali ilipelekea majeruhi na uharibifu wa magari.
Ni kwamba Desemba 31, 2023 majira ya saa 1:50 asubuhi huko maeneo ya Mbembela Jijini Mbeya katika barabara ya Mbeya/Tunduma Gari T.428 DXD/T.860 BWM aina ya FAW ikiendeshwa na Dereva aliyefahamika kwa majina ya Msafiri Mohamed @ Mwawila ilikuwa imebeba “Conflakes na Mayonise” likitokea Dar es Salaam kuelekea Lumbumbashi Kongo ambaye alikimbia mara baada ya ajali aligonga Gari T.287 DGK aina ya Toyota Hiace daladala inayofanya safari kati ya Stendi Kuu/Mbalizi iliyokuwa ikishuka kuelekea Mbalizi na kisha kugonga Gari T.163 DDA aina ya Sienta iliyokuwa ikiendeshwa na Daud Michael @ Mwasote [38] Mkazi wa Kalobe.
Aidha, Gari hilo liliendelea kugonga Gari namba T.977 DBN aina ya Toyota Hiace inayofanya safari kati ya Stendi Kuu/Mbalizi iliyokuwa imepaki Stendi ya Mbembela ikisubiri abiria iliyokuwa ikiendeshwa na Frank Filbert [34] Mkazi wa Iyunga na kugonga Gari nyingine ubavuni nyuma kushoto namba T.595 ECU/T.336 ECS Howo iliyokuwa ikiendeshwa na Lusekelo Jacob @ Mwanjala [46] Mkazi wa Vetenary Dar es Salaam aliyekuwa amepakia nondo kuelekea nchini Kongo na kusababisha uharibifu wa magari yote manne na majeruhi kwa watu watano.
Majeruhi katika ajali hiyo wametambulika kuwa ni 1. Neema Mwakisambe [23] Mkazi wa Nzovwe 2. Selina Ngonyani [31] Mkazi wa Sokomatola 3. Tunazael Elikunda [58] Mkazi wa Ghana 4. Upendo Sembalakane [54] Mkazi wa Sokomatola na 5. Steven Sinkwembe [40] Dereva wa Gari Toyota Hiace, Mkazi wa Iwambi. Chanzo cha ajali ni uzembe wa Dereva kushindwa kulimudu Gari lake katika eneo lenye mteremko baada ya kufeli breki. Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Jitihada za kumtafuta mmiliki wa Gari ili kuhamisha mzigo kwenye Gari jingine zinaendelea pia kusaidia kumpata Dereva aliyehusika katika ajali hii. Aidha ulinzi na usalama umeimarishwa eneo la tukio.Imetolewa na:BENJAMIN KUZAGA – ACPKamanda wa Polisi,Mkoa wa Mbeya.