Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Ndugu Mabara Mlolwa amewaongoza waombolezaji kushiriki mazishi ya aliyekuwa mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ya Ilemela Marehemu Dominick Kajara Sengo aliyefariki kwa ajali ya kugongwa na gari eneo la Kwa Malulu wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza siku ya Jumatatu ya Desemba 25, 2023
Akizungumza wakati wa kutoa salamu za rambi rambi kwa familia ya marehemu, Shughuli iliyofanyika katika viwanja vya nyumba ya familia ya marehemu iliyopo wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti huyo amemuelezea marehemu kama mtu asiyejikweza na aliyependa kushirikiana na makundi yote ya watu katika jamii bila kujali hali zao au tofauti nyengine ya aina yoyote.
‘.. Mara kadhaa akitokea Mwanza kuja Kahama Shinyanga au akitokea Kahama kurudi Mwanza ilikuwa lazima apite ofisini kutusalimia na mtapata wasaa kubadilishana mawili matatu, Mtu yeyote ataekukuta lazima tu atakusemesha ..’ Alisema
Aidha Ndugu Mlolwa amewataka viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuiga mazuri ya marehemu na kuyaendeleza huku akiwashukuru wana CCM kutokea mkoa wa Mwanza wilayani Ilemela hasa Mbunge wa Jimbo hilo Dkt Angeline Mabula kwa namna walivyojitoa kuhakikisha wanamsitiri mtoto wao
Nae Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kahama Ndugu Thomas Myonga amemuelezea marehemu kama mtu aliyekuwa mzalendo, mkweli na mpenda haki aliyeweka mbele maslahi mapana ya chama chake na Serikali huku akiwapongeza watu wa Ilemela na Mwanza kwa kumuamini na kumchagua kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika kipindi cha uhai wake akiwa Ilemela jijini Mwanza
Dominick Kajara Sengo amezikwa wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga makaburi ya wakristo ambapo mazishi yake yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Kahama mjini, mbunge wa Kahama vijijini, Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Katibu wa UVCCM wilaya ya Ubungo, wajumbe wa halmashauri kuu za CCM kutoka mkoa wa Mwanza na Shinyanga, wajumbe wa halmashauri kuu za CCM wilaya na wengineo wengi
Bwan ametoa, Bwana ametwaa, Jina la Bwana Lihimidiwe