Meneja wa Ruwasa mkoa wa Lindi Mhandisi Muhibu Lubasa akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji katika mkoa huo ofisini kwake mjini.
…………………………..
Na Muhidin Amri,
Nachingwea
WANANCHI wa vijiji vitatu vya Mpiluka A,Mpiluka B na Libeya kata ya Mpiluka Halmashauri ya wilaya Nachingwe mkoani Lindi,wameanza kupata huduma ya maji ya bomba kwa mara ya kwanza tangu nchi ipate Uhuru.
Ni baada ya serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya ya Nachingwea ,kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji ya bomba uliogharimu Sh.milioni 460.
Kukamilika kwa mradi wa maji Mpiluka,ulioanza kutoa huduma kwa wakazi 4,250 wa vijiji hivyo kumeleta nafuu kubwa kwa wananchi ambao kwa muda mrefu walitembea takribani kilomita 3 kila siku kwenda kuchota maji kwenye mito na makolongo.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Nachingwea Mhandisi Timotheo Kitinga alisema,ujenzi wa mradi huo umekamilika kwa asilimia 95 na umeanza kutoa huduma kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Alisema,mradi wa maji Mpiluka ulianza kutekelezwa mwezi April 2023 na unatekelezwa kwa njia ya mkandarasi ambapo kazi zinazotekelezwa ni ujenzi wa tenki la lita 100,000,kuchimba mitaro na kulaza mabomba umbali wa kilomita 6.6.
Alitaja kazi nyingine zinazoendelea kutekelezwa ni kujenga vituo vya kuchotea maji kwenye taasisi za serikali na kwenye maeneo ya wananchi na kuleta kupeleka umeme kwenye chanzo cha na kujenga ofisi ya Jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO).
Naye meneja wa Ruwasa mkoa wa Lindi Muhibu Lubasa alisema,wakati Ruwasa inaanzishwa mwaka 2019 upatikanaji wa huduma ya maji katika mkoa huo ilikuwa asilimia 58,lakini kwa muda wa miaka minne wamefanikisha kuongeza huduma hadi kufikia asilimia 68.1.
Kwa mujibu wa Lubasa,kutokana na utendaji kazi na maboresho makubwa yaliyofanyika katika kipindi cha miaka minne wamefanikiwa kutekeleza jumla ya miradi 60 kati ya hiyo miradi 40 imekamilika na 20 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake.
Aidha alisema,mwaka wa kwanza 2019/2020 walipokea jumla ya Sh.bilioni 11, 2020/2021(bilioni 6)2021/2022(bilioni17) na mwaka 2023/2024 wametengewa Sh.bilioni 10 kati ya hizo Sh.bilioni 7 zimeshapokelewa.
Alisema,lengo la Ruwasa mkoa wa Lindi ifikapo mwezi Disemba 2024 kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa wananchi kwa asilimia zaidi ya 80 wanaoishi maeneo ya vijijini.
“nimezungumzia miradi 60 lakini kuna miradi mingine zaidi ya 20 tunaendelea kuitekeleza katika maeneo mbalimbali ikiwemo mradi mkubwa wa kimkakati ambao utakamilika mwezi februari 2025,mradi ule ukikamilika tuna uhakika wa kufikisha asilimia 85 ya utoaji wa huduma ya maji vijijini”alisema Lubasa.
Diwani wa kata ya Mpiluka Daud Mkane alisema,kukamilika kwa mradi huo kumewaondoa mateso makubwa wananchi w vijiji hivyo kwenda hadi kata za jirani kufuata maji kwa ajili ya matumizi yao.
Amewapongeza wasimamizi wa mradi huo wataalam kutoka ofisi ya Ruwasa wilaya ya Nachingwea,kwa usimamizi mzuri na kukamilika kazi kwa wakati na hivyo kuwezesha wakazi wa kijiji hicho kupata maji ya bomba kwa mara ya kwanza.
Mkazi kijiji hicho Anastanzia Tamba alisema,kwa muda mrefu walilazimika kutumia maji ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu kwa kuwa yalitumika pamoja na wanyama wakiwemo nguruwe pori.
Ameiomba Ruwasa kuboresha huduma zake kwa kutafuta vyanzo vingine vyenye maji baridi,kwani yaliyopo hayana radha kwa kuwa yana asili ya chumvi.