Na Issa Mwadangala
Kamanda wa Polisi Mkoa wa songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Theopista Mallya Disemba 29, 2023 ameendelea na operesheni ya ukaguzi wa magari ya abiria kwenye barabara ya kwenda Mbeya Tunduma katika kituo cha ukaguzi wa magari Mahenje wilayani Mbozi.
Katika opereshion hiyo kamanda Mallya amemfutia leseni dereva Ally Lugenge (56) akiwa anaendesha gari lenye namba za usajili T855 DXL Kampuni ya Masihi inayofanya safari zake Ubaruku-Mbeya-Tunduma na Ileje.
Gari hilo aina ya Fuso yenye uwezo wa kubeba abiria 45, ambapo kondakta na dereva wa gari hilo walipakia abiria zaidi ya 66 pamoja na mizigo kitu ambacho ni kinyume na taratibu za sheria za usalama barabarani pia ni hatari kwa usalama wa abiria.
Kamanda Mallya amechukua uamuzi wa kumfutia leseni dereva huyo baada ya kurudia kosa ambalo alilifanya jana la kuzidisha abiria ambapo alipewa onyo kali kisha kutozwa faini lakini dereva huyo alirudia kosa lilelile ambalo lilimpelekea Kamanda Mallya kumfutia leseni dereva huyo.
Sambamba na hilo Kamanda Mallya amewakamata makondakta wawili wa mabasi madogo ya abiria kwa kosa la kuchanganya abiria na mizigo kwenye gari la abiria ambalo ni kosa kwa sheria za usalama barabarani, makondakta hao ni Frank Dicksoni (24) pamoja na Zakayo Msimwa (21).
Kamanda Mallya ametoa wito kwa madereva na makondakta kufuata sheria za usalama barabarani bila Shuruti pia aliwataka abiria kujisimamia wenyewe pindi waonapo gari limejaa wanatakiwa wasipande na sio mpaka wamuone askari ndio watii sheria za usalama barabarani kila mmoja anatakiwa kutimiza wajibu wake ili kupunguza ajali ambazo zinaepukika.