Dkt. George Dilunga, akizungumza na watoto wanaoishi katika Makao ya Kitaifa ya Kulelea Watoto Kikombo. Watumishi wa Idara ya Magonjwa ya Dharura wa Hospitali ya Benjamini Mkapa katika picha ya Pamoja na watoto wanaolelewa kwenye Makao ya Taifa ya Kulelea watoto Kikombo.
…………………..
Na Raymond Mtani BMH
Jamii imeaswa kuwatembelea Watoto wanaolelewa katika Makao ya Kulelea Watoto ili kuwajenga kisaikolojia kwa kuwa wengi wa Watoto hao wanatoka katika mazingira yenye historia ngumu.
Wito huo umetolewa na Jonas Tarimo, Meneja wa Makao ya Taifa ya Kulelea Watoto Kikombo jijini Dodoma, alipokuwa akitoa taarifa kuhusu shughuli za Makao hayo kwa Wafanyakazi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa waliyofika kutoa mkono wa Sikukuu mwishoni mwa wiki.
“Watoto hawa wanatoka katika uzoefu mgumu, ndoa zenye migogoro, unyanyasaji na wengine hawana familia kabisa, hivyo mnapofika hivi wakaona sura mpya, mkaongea nao, mnatusaidia sana kuwajenga kisaikolojia” Alisema Tarimo.
Aidha, Tarimo alisisitiza kuwa, msaada ni muhimu ingawa kufika katika vituo hivyo ni muhimu zaidi kwa kuwa ni Watoto wa jamii, kuongea nao hupanua mawanda ya uelewa wao na kuwapa mtazamo mpya wa maisha.
Dkt. George Dilunga, Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Mkuu wa Idara ya Magonjwa hayo BMH, anasema kuwa hatua ya kutembelea Makao ya Kitaifa Kikombo inafuatia uhusiano uliyopo baina ya taaisi hizo mbili.
“tumekuwa tukitoa huduma za Afya kwa Watoto wanaoishi hapa kwa kuwafanyia uchunguzi na matibabu kila baada ya miezi mitatu tangu Juni 16, 2021 yalipozinduliwa Makao haya hivyo wamekuwa sehemu ya familia yetu” alisema Dkt. Dilunga.
Dkt. Dilunga aliongeza kuwa, uamuzi wa kujumuika nao msimu huu wa Sikukuu, ulilenga kuongea na Watoto hao kama sehemu ya kuwapa faraja msimu huu wa sikukuu.
BMH ilikabidhi Nguo, Jora la kushona sare za shule, seti maalumu kukidhi mahitaji ya shule iliyohusisha Daftari, Kalamu na Rula kwa Watoto zaidi ya 80 ambayo ni michango ya wafanyakazi wa Idara ya Magonjwa ya Dharura wa BMH.
Ifahamike kuwa, kuna zaidi ya Watoto 24,000 wanaolelewa katika makao zaidi ya 320 yaliyosajiliwa katika sehemu mbalimbali nchini, Watoto hao ni zao la migogoro ya ndoa, unyanyasaji, vifo vya wazazi, Watoto kutelekezwa miongoni mwa sababu nyinginezo.