RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Uwanja wa Amaan Zanzibar, baada ya kukamilika ujenzi wake, ufunguzi huo uliofanyika leo 27-12-2023 ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu)
………
Na Khadija Khamis – Maelezo. 27/12/2023.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya michezo ili kuibua fursa na vipaji vilivyopo.
Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanja ”Amani Comples” baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa, ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar ameahidi kuimarisha sekta ya michezo nchini.
Alisema Serikali itaendelea kuchukuwa hatua mbali mbali ili kuimarisha michezo kwa lengo la kuwapatia vijana ajira.
“Hatua imeanza ya upimaji na uchoraji wa ramani na kwa kila wilaya kutakuwa na viwanja mchanganyiko vya michezo.” alisema Dkt. Mwinyi.
Amewataka wananchi kuzingatia umuhimu wa michezo kwani michezo hujenga, uzalendo, ushirikiano, upendo na udugu.
Alieleza kuwa ujenzi wa uwanja wa Amani na Gombani Pemba ni miongoni mwa utekelezaji wa dhamira ya serikali pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020 – 2025 na Sera ya michezo katika kuhakikisha sekta ya michezo inaimarika nchini.
Aidha amesema hali hiyo itaweza kuimarisha sekta ya michezo na kutoa manufaa ya kiuchumi kwa faida ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.
Alifahamisha kuwa ujenzi huo ni uwamuzi wa serikali kwa lengo la kuimarisha sekta ya michezo hivyo serikali itaendelea kujenga miundombinu hiyo kwa kila Wilaya.
Nae Waziri wa Habari Utamaduni na michezo Mh.Tabia Maulid Mwita amesema ukarabati mkubwa wa Uwanja wa mpira Amani Complex na kuwa na hadhi ya viwango vya mpira miguu Duniani (FIFA) ambapo amesema umeleta faraja kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Zaidi ya Sh. bilioni 56 zimetumika katika kufanya ukarabati wa kiwanja hicho na kuendelea kujenga viwanja vyengine mbali mbali.