Na John Walter-Manyara
Hadi kufikia sasa misaada mbalimbali inayoendelea kutolewa na wadau mbalimbali wilaya ya Hanang’ mkoa wa Manyara palipotokea maafa ya maporomoko ya tope, mawe na magogo ina thamani ya shilingi bilioni 2,583,306,997.00 na fedha taslimu shilingi 5,208,729,711.00.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi katika taarifa yake ya desemba 24, 2023, Fedha taslimu zinajumuisha shilingi bilioni 2.5 zilizoletwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na shilingi 2,708,729,711.00 zilizomo kwenye akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Misaada ya Maafa inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kati ya fedha hizo, kiasi cha sh. 2,289,260,025.00 zimechangwa na taasisi na mashirika ya umma kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na kiasi kilichobaki cha sh. 419,469,152.00 kimechangwa na wahisani mbalimbali.
Serikali inaeendelea kuwashukuru Watanzania kwa utu, upendo, uzalendo na moyo wa kujitolea ambao umesaidia kupatikana kwa chakula cha kutosha na mahitaji muhimu ili kuwasaidia waathirika kuendelea na maisha yao na kusisitiza wanaoendelea kuleta misaada kujikita zaidi katika vifaa vya ujenzi.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa Kambi tatu zilizokuwa zinatoa huduma zimefungwa baada ya waathiriwa wote 690 kutoka kaya 140 kurejea makwao na kwa ndugu zao.
Ikumbukwe kuwa Waathirika 534 walikuwa wakilala kambini na 156 walikuwa wakija asubuhi na kuondoka jioni.
Utaratibu wa kugawa misaada hiyo unaoratibiwa na Idara ya Maafa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikishirikiana na uongozi wa mkoa wa Manyara na wilaya ya Hanang pamoja na kamati zao za usalama, unatumia watalaam kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Kuhusu Mgawo wa misaada , taarifa imeeleza kuwa unalenga kwanza waathirika 1,292 waliothibitika kupoteza nyumba zao ama kuharibika au kuingia tope. Idadi hii ilipatikana baada ya tathmini ya kina ya picha za satelaiti, rekodi za sensa, ukaguzi halisi wa nyumba hadi nyumba na rekodi za serikali za mitaa katika ngazi ya vitongoji, vijiji na kata.
Utaratibu wa ugawaji misaada umewekwa kwa kubandika majina ya waathirika kwenye ofisi za kata baada ya kukamilika kwa tathmini ambapo mhusika akifika huelekezwa kituo chake cha kupokelea misaada.
Tangu wiki iliyopita wananchi wamekuwa na ratiba za kwenda kupokea misaada kila siku kutokana na wingi wa misaada hiyo. Kwa wastani kila kaya inapata chakula cha kutosha miezi sita au zaidi ambapo kwa baadhi ya bidhaa kama sukari wananchi hao wanapewa ya kutosha kutumia kwa zaidi ya miaka miwili kwa mujibu wa vipimo vya lishe.
Misaada inayotolewa ni chakula cha mahindi, ngano, mchele, unga wa mahindi, unga wa ngano, maharage, mafuta ya kula, maziwa, unga wa lishe kwa watoto, mayai, sabuni, magodoro, mablanketi, mashuka, mikeka, ndoo, majiko ya kupikia ya gesi na mitungi yake, masufuria, nguo, viatu, kandambili na vingine vingi.
Idadi ya watu waliopoteza maisha imebakia kuwa 89 tangu tarehe 11 Desemba na mwili mmoja wa mtoto wa kike bado haujatambuliwa. Maafa haya yalitokea alfajiri ya tarehe 3 Desemba, 2023, baada ya maporomoko ya tope, mawe, magogo na maji kutoka mlima Hanang kuvamia vijiji vinne vilivyokuwa kando ya mlima Hanang na kata nne za mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang.
Hadi sasa majeruhi wanne bado wanatibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara iliyopo mjini Babati na mmoja amepelekwa Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma. Serikali imegharamia matibabu, mazishi na kutoa mkono wa pole kwa wafiwa. Majeruhi wote walifikia jumla ya 139.
Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa akaunti ya kielektronikia kuchangia fedha za misaada yenye nambari 9921159801 iliyopo Benki Kuu ya Tanzania na inayopokea fedha kupitia benki yoyote nchini na pia kutoka nje ya nchi kwa kutumia swift code ya TANZTZTX. Miamala yote inatakiwa kuwa na maelezo MAAFA HANANG.