Na Fauzia Mussa, Maelezo Zanzibar
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar inatarajia kunufaika na fedha zilizotolewa na Tume ya Taifa ya sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kuendeleza tafiti katika taasisi mbalimbali Nchini.
Akizungumza kuhusiana na fedha hizo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI) Dkt. Mohammed Dhamir Kombo amesema Jumla ya dola za Kimarekani 250,000 zimetolewa na tume hiyo ili kuendeleza tafiti zinazofanywa na taasisi mbalimbali ikiwemo taasisi hiyo ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar .
Alisema Taasisi hiyo inatarajia kufanya tathmini juu ya changamoto za uzalishaji wa zao la karafuu kupitia fedha hizo, kufuatia agizo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kuitaka Tume ya Mipango Zanzibar kutathmini nakujua changamoto za uzalishaji wa zao hilo.
“ZARI tutazitumia fedha hizi katika kuangalia, kuchunguza na kuchambua sababu zinazopelekea zao la karafuu kurudi nyuma” alisema Dkt. Mohammed
Alieleza kuwa utafiti huo utaangalia viashiria na changamoto za kupungua kwa uzalishaji wa karafuu, pamoja na kutoa mbinu bora za kutatua changamoto zitakazopelekea kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji, kuliongeza thamani zao hilo na kuleta tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.
Alifahimisha kuwa awali zao hilo lilizalisha zaidi ya tani elfu 30 na kwa mwaka 2022 lilizalisha tani 8736 na kuingiza kiasi cha shilingi bil.144.9 kwa mwaka.
Nae Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt.Amos Nungu amesema tume hiyo imekuwa ikitafuta fedha kwa wadau mbalimbali ili kuendeleza matokeo ya tafiti zinazofanyika nchini ili kuweza kuingia sokoni.
“fedha hizi zimetolewa na Nchi ya uiengereza kwa nchi 17 ambazo tafiti hizo zinaweza kushirikiana, na matokeo hayo kuweza kutumika nchi nyengine” alisema Dkt.Amos
Aidha alifahamisha kuwa Serikali imetoa fedha hilo ili kulifanyia utafiti zao la karafuu baada ya tume ya mipango Zanzibar kulifanyia tathmini na kuona kuwa kila mwaka tija ya zao hilo imekua ikipungua .
Jumla ya Taasisi nne zinatarajia kunufaika na fedha hizo ikwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI), Chuo cha kilimo Sokoine (SUA), Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kibaha na Taasisi ya Utafiti wa viumbe bahari Tanzania (TAFIRI).