Baadhi ya vyombo vya usafiri ikiwemo Bajaji zikianza kupita katika barabara hiyo inayojengwa na wakala wa barabara za mijini na vijijini(TARURA)Wilaya ya Mbinga kwa gharama ya Sh.milioni 470.……………………………….
Na Muhidin Amri, Mbinga
WAKALA wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,umeanza kujenga barabara za lami na kufungua barabara mpya ili kuwezesha wananchi kufika kusiko fikika katika Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani humo.
Miongoni mwa barabara hizo ni Barabara ya Kigonsera-Hospitali ya wilaya yenye urefu wa kilomita 3.9 inayojengwa kwa gharama ya Sh.milioni 470 ambapo mita 700 zimeanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
Meneja wa Tarura wilaya ya Mbinga Mhandisi Oscar Mussa ameeleza kuwa,ujenzi na ufunguzi wa barabara hizo ni mpango maalum wa serikali ya awamu ya sita kupitia Tarura kuhakikisha maeneo yote yanapitika na kufikika kwa urahisi.
Kwa mujibu wa Mussa,barabara hiyo na nyingine zinazoendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali wilayani Mbinga,zitatoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya,mkoa na Taifa kwa ujumla.
Alisema,barabara hiyo inatekelezwa na Tarura kwa fedha za mfuko wa Barabara nchini na inajengwa na Mkandarasi kampuni ya VAG Contructors na ilianza kujengwa mwezi Septemba mwaka huu na inatarajia kukamilika mwezi April mwakani.
Alitaja,kazi zinazotekelezwa ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami,ujenzi wa mitaro pande zote za barabara na kufunga taa 10 za barabara ili kurahisisha usafiri wa wananchi wanaokwenda Hospitali ya wilaya kupata matibabu.
Aidha alisema,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Tarura wilaya ya Mbinga imepanga kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 1.6 kwa kiwango cha lami,barabara za mawe urefu wa mita 400,kufungua barabara mpya kilomita 280,kukarabati na kujenga madaraja katika maeneo mbalimbali.
Pia alieleza kuwa,katika kipindi hiki cha mvua za masika wamefanikiwa kupitia zaidi ya madaraja 180 na kati ya hayo madaraja 8 yaliyo katika hali mbaya yamefanyiwa ukarabati wa haraka ili yaweze kupitia kwa urahisi.
Mkazi wa kijiji cha Kigonsera Kaltas Miti alisema,barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa sababu itawezesha kusafiri kwa urahisi kutoka sehemu moja hadi nyingine na pale wanapotaka kwenda Hospitali ili kupata matibabu.
Hata hivyo,ameiomba Tarura kukamilisha matengenezo ya mitaro haraka ili watoto wadogo waweze kupita kwa urahisi wanapotaka kwenda upande wa pili.
Richard Ndomba,ameishukuru Tarura kujenga barabara hiyo kwani itawasaidia kusafiri mazao kutoka shambani kwenda sokoni,badala ya wafanyabiashara kutumia fursa ya ubovu wa barabara kwenda moja kwa moja mashambani kununua mazao kwa bei ya hasara.
Half Kayombo mkazi wa Mbinga alisema,kujengwa kwa barabara ya lami,kutaongeza thamani ya maeneo yao na kuvutia watu wengi kwenda kuwekeza na kuhamasisha wenyeji kujenga nyumba bora na za kisasa.