Na Abel Paul, Jeshi la Polisi- Arusha.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema kuwa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea kuimarisha ulinzi ambapo limebainisha kuelekea sikukuu za krismasi na mwaka mpya litahakikisha sikukuu hizo zinasherekewa kwa amani na utulivu hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa huo ni kitovu cha utalii hapa nchini.
Akitoa taarifa hiyo kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amesema Katika kuhahkikisha sikukuu hizo zinasherehekewa kwa amani na utulivu Jeshi hilo litahakikisha linatoa ulinzi kwenye nyumba za ibada,kumbi za starehe Pamoja na maeneo mengine yote Katika Mkoa huo ambapo askari watapangwa katika doria za miguu, pikipiki, magari na doria za mbwa katika jiji la Arusha lakini pia Mkoa kwa ujumla.
Kmanda Masejo amewataka wazazi kuacha kuwapeleka Watoto kwenye kumbi za starehe maarufu (disco toto), pia amepiga marufuku kwa madereva kuendesha magari wakiwa wamelewa, huku akiwata wamiliki wa bar wazingatie masharti ya leseni zao ambazo zinaonyesha muda halisi wa kufunga, halikadhalika kwa wamiliki wa kumbi na maeneo mengine ya starehe wanapaswa kuzingatia usalama katika maeneo yao na kutojaza watu kupita kiasi.
ACP Masejo ametumia fursa hiyo kuwatakia wananchi wote wa Mkoa wa Arusha na wageni walifika katika Mkoa huo Kheri ya Krismas na Mwaka Mpya 2024 huku akiwakumbusha kauli mbiu isemayo ulinzi unaanza na mimi.
Sambamba na hilo amewapa angalizo kufanya vitu kwa kiasi, bila kuvuka viwango wala mipaka ambayo inaweza kusababisha wakaingia mwaka mpya wakiwa na changamoto zilizosababishwa na furaha iliyopitiliza.