Meneja mahusiano kitengo cha kilimo biashara Kanda ya ziwa Michael George akizungumza na waandishi wa habari
Wadau wa uvuvi wakiwa ukumbini kwenye kikao
………………………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Benki ya CRDB Kanda ya ziwa imetoa mikopo zaidi ya bilioni moja kwa mwaka 2023 kwaajili ya wavuvi wadogo wadogo ili waweze kukuza mitaji yao na kununua dhana mbalimbali za uvuvi.
Hayo yamebainishwa na Meneja mahusiano kitengo cha kilimo biashara Kanda ya ziwa Michael George, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye kikao kazi cha wadau wa uvuvi kilicho fanyika Jijini Mwanza.
George amesema kuwa wamewakopesha boti za kisasa zaidi ya 100 ili waweze kufanya shughuli zao za uzalishaji kwaufanisi.
Mbali na kuwapa mikopo hiyo wanawapa elimu ya kifedha ili waweze kutunza fedha kwenye taasisi za kifedha hatua itakayosaidia kuwa na nidhamu katika matumizi.
Aidha, amesema wanawashauri wavuvi wanaovua kwakutumia mitumbwi wabadilike ili waanze uvuvi wa kutumia njia ya vizimba.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti kamati ya ushauri uvuvi endelevu ziwa Victoria Hassan Muhenga, amesema bado kunachangamoto ya uvuvi haramu katika ziwa hilo hivyo ameiomba Wizara ya uvuvi na mifugo kusimamia sheria vizuri hatua itakayosaidia kutokomeza uvuvi huo.
Joshua Manumbu ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, amesema wameathirika na upungufu wa mazao ya samaki kutokana na uvuvi haramu unaofanyika ziwa Victoria huku akieleza mikakati waliyonayo ya kudhibiti uvuvi huo ikiwemo kutengeneza faiba boti.
“Tulipata fedha kutoka Serikali kuu milioni 400 na sisi kama Halmashauri tuliongeza milioni 100 tukatengeneza faiba boti tano pia tukakarabati faiba boti mbili zilizokuwepo ambazo zitatumika kudhibiti uvuvi haramu na utoroshaji wa mapato katika eneo letu”,amesema Manumbu