Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar mhe.Lela Muhamed Mussa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusuiana na Mapinduzi ya elimu huko Karume house kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi.
Mwandishi wa habari SN online tv Bakari Abdallah akiuliza swali kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar mhe.Lela Muhamed Mussa wakati akizungumzia Mapinduzi ya elimu kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya mapinduzi huko Karume house Mjini Unguju. (PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR )
………
Na Rahma Khamis Maelezo. 22/12/2023
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh Lela Muhamed Mussa amesema Serikali imetiliana saini na Wahisani mbalimbali ikiwemo Marekani ili kuleta mageuzi ya elimu nchini.
Akizungumzia mafanikio ya Wizara hiyo amesema Serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha ubora wa elimu hasa kwa upande wa sayansi na ufundi ili kuleta maendeleo.
Amesema jumla ya dola 61 za kimarekani zimetumika kusaidia uboreshaji wa sekta ya elimu pamoja na kujenga chuo cha sayansi Bweleo Wialaya ya Magharibi “B”.
Aidha Waziri lela amefahamisha kuwa Serikali ya awamu ya 8 imfanikiwa kuwaajiri walimu wapya 160 kwa kipindi cha miaka mitatu na inatarajia kuajiri waalimu 1500 ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa waalimu.
Vile vile Skuli 34 za Ghorofa zimeshakamilika katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwa muda mmoja na kuondosha usumbufu wa kwenda mara mbili kutafuta elimu katika Skuli zao.
Amefahamisha kuwa Wizara itajenga vyuo 5 vya amali ikiwemo chuo cha ubaharia Maruhubi kwa ajili ya kuwajengea uwezo Wanafunzi pamoja na Maabara ya Kisayansi kwa lengo la kuimarisha ufahamu kwa Wanafunzi.
Ameongeza kuwa kabla ya Mapinduzi kulikua hakuna Chuo kikuu hata kimoja lakini baada ya Mapinduzi hadi sasa Vyuo vikuu 7 vimejengwa katika maeneo tofauti ikiwemo SUZA, IPA, na Mwalimu na Nyerere hali ambayo inapelekea kuongezeka idadi ya Wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu.
Amesema Wizara imefanikiwa kujenga Skuli mbili za wananfunzi wenye mahitaji maalumu katika maeneo ya Jendele na Pujini ili kuwaondolea usumbufu wanafunzi hao jambo ambalo litapelekea kupata kusoma wanafunzi wote wenye ulemavu kusoma katika Skuli za Serikali .
“Kipaombele chetu kwa wanafunzi ni kuweka grains floo katika skuli zote pamoja na kuwajengea vyoo maalumu ili wasipate shida wanafunzi wetu”alifafanua Waziri huyo
Akizungumzia kuhusu kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi , ameeleza kuwa umeongezeka na kufikia hadi asilimia 65.9 kwa kidato cha sita kwa wanafunzi sayansi jambo ambalo ni kubwa ukilinganisha na kabla ya Mapinduzi ya mwaka 64.
Hata hivyo Waziri Lela amebainisha kuwa Wizara imeweka mradi maalumu wa wakipita katika jamii na kuangalia wanafunzi ambao wamekatisha skuli na kuwarejesha pamoja na kuwapima ufahamu wao kwa ajili ya kuanza masomo ili kufikia lengo la Serikali la kila mwanafunzi apatiwe elimu.