Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa ifikapo mwezi Januari, 2024 Ofisi yake ya Mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Mbeya wamekusudia kumaliza changamoto za elimu katika shule zote 83 za Msingi ikiwemo ukarabati wa miundombinu, madawati pamoja na vyoo.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 22 Disemba, 2023 wakati wa Mkutano wake na Mabalozi na Wenyeviti wa Serikali za mitaa wa Jimbo hilo. Mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Mjini umelenga kuwakumbusha Mabalozi na Wenyeviti hao kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM Jimboni humo.
Sambamba na hayo, Dkt. Tulia amesema kuwa kupitia Ofisi yake amepanga kuwasaidia watoto wanaosoma katika mazingira magumu kwa kuwawezesha mahitaji yao mbalimbali ikiwemo nguo za shule na madaftari kwa lengo la kuchochea kasi ya maendeleo ya elimu katika Jimbo lake.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM taifa (NEC) anayewakilisha Mkoa wa Mbeya Ndg. Ndele Mwaselela, amemshukuru na kumpongeza Dkt. Tulia kwa jitihada zake za kutatua changamoto za Wananchi wake ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakikosa mchango huo ambapo amewataka pia Wananchi hao wamlinde kwa uchu mkubwa.