Waziri wa Ardhi na maendeleo ya makaazi Mhe. Rahma Kassim Ali akitoa taarifa kuhusiana na Mapinduzi ya sekta ya Ardhi na maendeleo ya makaazi kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi, huko Karume House
……….
NA SHEHA SHEHA, MAELEZO-20-12-2023.
Waziri Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe. Rahma Kassim Ali amesema Serikali inaendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa kufuata Sheria za ardhi ili kuepukana na migogoro isiyo ya lazima kwa wananchi.
Waziri Rahma amesema hayo leo katika Ukumbi wa ZBC, Karume House. wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mikakati, malengo na mafanikio ya Wizara hiyo Kuelekea madhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kupitia njia mbali mbali juu ya umuhimu wa kufuata Sheria za ardhi ili kuepukana na vichocheo vinavyopelekea migogoro ya ardhi isiyo ya lazima Nchini.
Amesema Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi inaendelea kuweka Mifumo ya kidigitali ili kurahisisha upatikanaji huduma kwa jamii na kuziba mianya ya rushwa na upotevu wa mapato Nchini.
Amesema, Serikali imekamilisha uthamini wa mali kwa ajili ya ulipwaji wa fidia ili kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo Miradi inayosimamiwa na Shirika la Umeme, Mamlaka ya Maji, Ujenzi wa Masoko makubwa, Ujenzi wa Hospitali kubwa za Mikoa na Wilaya, Ujenzi wa Barabara na upanuzi wa viwanja vya Ndege Unguja na Pemba.
Amefahamisha kuwa Serikali imeweka utaratibu mzuri wa uhaulishaji ardhi na kufanikiwa kupunguza muda wa huduma za uhaulishaji wa ardhi kutoka siku 30 hadi siku 15 baada ya taratibu na vielelezo kukamilika ili kupunguza usumbufu kwa wananchi.
Waziri Rahma amesema Serikali imeanzisha Kamisheni hiyo yenye Lengo la kusimamia masuala yote ya ardhi pamoja na kuziunganisha taasisi zinazosimamia matumizi na maendeleo ya ardhi ili kuleta usimamizi bora Nchini.
Amefahamisha kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mipango ya Matumizi ya Ardhi, ikiwemo Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Ardhi, Mpango Mkuu wa Matumizi ya Ardhi pia inaendelea kupanga Mipango ya miji midogo midogo kwa Unguja na Pemba ili kuitumia Ardhi kwa ufanisi.
“Serikali imefanikiwa kupima ardhi ya akiba katika zoni tano pamoja na kukamilisha upangaji wa maeneo ya Nungwi, Mkokotoni, Chwaka, Dunga, Mahonda na Makunduchi.” Alisema Waziri Rahma.
Hata hivyo amesema Serikali imeweka Sera na Sheria mbali mbali za kusimamia masuala ya Uwekezaji katika Sekta miliki na kuruhusu wafanyabiashara kuingiza vifaa vya ujenzi wa nyumba pamoja na kutoa Msamaha wa Kodi kwa Wawekezaji ili kuwasaidia wananchi kupata Makazi bora kwa urahisi.
Hafla hiyo ikiwa ni muendelezo wa mahojiano baina ya Mawaziri wa Wizara mbali mbali na Waandishi wa Habari katika kuelezea maendeleo, malengo na mafanikio ya Wizara, kuelekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.