Umoja wa Wenza wa viongozi “New Millenium Women Group” wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyokabiliana mafuriko yaliyosabisha maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang, Mkoani Manyara.
Akizungumza na waathirika katika kambi iliyopo shule ya sekondari Katesh, Wilayani Hanang Mkoani Manyara kwa Mlezi wa Umoja huo ambaye ni mke wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mama Mary Majaliwa amesema kitendo cha Rais Dkt. Samia kuacha majukumu yake tena akiwa nje ya nchi na kurejea kwenda kuwapa pole waathika, ni kitendo cha upendo mkubwa alionao kwa Watanzania.
Mama Majaliwa amesema hayo jana (Disemba 18, 2023) wakati akizungumza na Waathirika wa maafa hayo kwa niaba ya wenza wengine wa viongozi. Mafuriko hayo yamesababisha vifo vya watu 89 na wengine zaidi ya 600 kukosa makazi katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara.
“Tumeguswa sana na madhila yaliyowapata na tumekuja kuwapa pole lakini pia tumekuja kuungana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na tunamshukuru kwa namna alivyoweza kukabiliana na matokeo ya janga hili na kuhakikisha waathirika wote wanapata huduma kwa haraka kwa kuleta Serikali yake hapa na tunashukuru kuona Hanang imetulia, na shughuli zinaendelea kuimarika.”
Msaada walioutoa ni pamoja na sare za shule 200, viatu jozi 216, madafutari 611, blanketi 105, mashuka 105, chupi za watoto 600, vitenge 40, kanga 100, mchele kilo 450 vifaa vingine na vyandarua, tisheti na taulo za kike.
“Muendelee kuishi kwa upendo, saidianeni kwa hali na mali huku mkimtanguliza Mungu kwa kila hali, pia tunaomba Serikali ikikamilisha miundombinu ya shule, iliyopata athari muwapeleke watoto shuleni, msiwaache nyumbani.”
Naye Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu Fredreck Sumaye mama Esther Sumaye ameishukuru Serikali kwa namna ilivyosaidia waathirika na kuomba waendelee na huduma kwa wathirika wachache waliobaki.
Awali akitoa taarifa ya janga hilo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema idadi ya waathirika kwenye kambi imepungua kutokana na juhudi zilizofanywa na serikali kuwaunganisha waathirika na ndugu zao na kwenye kambi wamebaki waathirika 27.
“Tulikuwa tunakambi tatu za waathirika, moja ikiwa Ganana, Gendabi na Katesh na tulikuwa na waathirika jumla 683 na Serikali imekuwa ikiwahudumia tangu kutokea kwa janga hili, lakini kadri siku zinavyokwenda, baadhi ya waathirika walikuwa wakiomba kutoka baada ya kupata ndugu zao na waliosema wanataka kwenda Mwanza kwa ndugu zao, Serikali iliwagharamia”
Aliongeza kuwa waathirika ambao waliwapata ndugu zao wilayani Hanang na maeneo ya jirani pia serikali iliwagharamia usafiri na kuwapeleka kwa ndugu zao pamoja na kupewa mahitajikutosha mwezi mzima.
“kila wakati tumeendeea kuwafuatilia kuona wanaendeleaje kwa sababu zoezi linalofuata ni kuhakikisha wanarudi kwenye makazi yao yatakayokuwa yameandaliwa ili warejee katika maisha yao kama kawaida.”
Tayari shughuli za kijamii zimerejea kwa kiasi kikubwa katika mji wa KATESH baada ya barabara kuu na zile za mitaa kufunguliwa na kazi inayoendelea ni kutoa tope lililojaa ndani ya makazi huku wataalamu wakiendelea kufanya tathmini ya uharibifu uliosababishwa na maporomoko hayo.