Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Katika kuhakikisha elimu ya afya inafika kila mahali na kwa ufasaha Shirika la Save the Children limekabidhi vipaza sauti pamoja na tochi kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kutoka kata zilizoathiriwa na Mafuriko Wilayani Hanang mkoani Manyara .
Akizungumza mara baada ya makabishiano ya vifaa hivyo, Mganga Mkuu Halmashauri ya Hanang Mkoani Manyara Dkt.Mohamed Kodi amesema vifaa hivyo ikiwemo vipaza sauti vitawasaidia Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii katika kutoa elimu ya afya ikiwemo umuhimu wa kutibu maji ya kunywa kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
“Vifaa hivi vitasaidia Wahudumu afya Ngazi ya Jamii kutangaza na kutoa elimu wanapopita mitaa kwa mitaa na nyumba kwa nyumba hususan umuhimu wa kutumia dawa ya kutibu maji ya kunywa katika kudhibiti magonjwa ya mlipuko na ujumbe utafikia watu wengi kwa wakati mmoja ”amesema.
Kwa upande wake mwakilishi wa Save the Children Wiliam Nkuhi amesema vitendea kazi hivyo pia vitasaidia katika utoaji wa huduma za ulinzi wa mtoto na msaada wa Kisaikolojia ambapo pia tochi hizo zitawasaidia Wahudumu wa Afya Ngazai ya Jamii kufanya kazi za usiku pale inapopidi.