………………
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, ameeleza kuwa maghala ya mbolea nchini yana shehena ya kutosha kutumika msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024.
Amewataka wakulima kuendelea kujitokeza kujisajili pamoja na kuhuisha taarifa zao ili waweze kunufaika na mbolea za ruzuku kwa kununua kwa wakati kwani mbolea imekwisha sambazwa mpaka maeneo ya vijijini ambapo wakulima wanaruhusiwa kuendelea kununua na kuhifadhi kwa matumizi ya baadaye.
Laurent amesema hayo mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya kukagua maghala ya wafanyabiashara wa mbolea katika Jiji la Dar es Salaam iliyolenga kujionea kiasi cha mbolea kilichopo na kujiridhisha na utendaji wa kampuni hizo endapo unazingatia kanuni na sheria za kujihusisha na biashara ya mbolea nchini.
Amesema, pamoja na kujiridhisha na uwepo wa mbolea za kupandia na kukuzia katika maghala ya mbolea ya waingizaji wa mbolea nchini, Laurent amesema kuna meli iliyopakia shehena ya mbolea ya kukuzia kiasi cha tani elfu 20 imekwisha tia nanga tayari kwa kupakua mbolea zitakazosambazwa kwa wakulima nchi nzima.
Pamoja na hayo, Laurent alikutana na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za kujihusisha na biashara ya mbolea kwa baadhi ya kampuni na kuzitaka kampuni hizo kusitisha shughuli zao mpaka pale watakapokamilisha vigezo vya kufanya shughuli hizo ikiwa ni pamoja na kuzingatia uvaaji wa vifaa vya usalama ili kutunza afya za wafanyakazi wao.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wengine wa mbolea Jijini humo, Brijesh Barot, Mtendaji Mkuu wa Kampuni la mbolea la Premium Agro Chem ltd ameiomba Serikali kuzipa kipaumbele meli za mbolea zinapofika bandarini ili kushusha shehena za mbolea kwa wakati na kuzifikisha kwa wakulima.
Amesema, ucheleweshwaji wa kushusha mzigo bandarini unapelekea kuongezeka kwa gharama zinazowanufaisha mataifa ya nje wanaolipwa kwa pesa za kigeni.
Katika ziara hiyo ya siku 2 tarehe 15 na 16 Desemba, 2023 Mkurugenzi Laurent aliandamana na Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Happiness Mbele, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya uzalishaji wa Ndani na ununuzi wa mbolea kwa pamoja na maafisa Udhibiti Ubora, Raymond Konga na Azizi Mtambo.