Na, Elimu ya Afya kwa Umma.
Wananchi wa Kijiji cha Sebasi Wilayani Hanang Mkoani Manyara wamehimizwa kuendelea kuzingatia kanuni za afya ikiwemo kutumia maji yaliyotibiwa na vidonge vya Klorine ili kuweza kuepuka magonjwa ya kuhara na kutapika.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Sehemu ndogo ya Maji na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya Anyitike Mwakitalima baada ya kutembelea katika kijiji Sebasi Wilayani Hanang Mkoani Manyara ikiwa ni mwendelezo wa kuhakikisha kanuni za usafi wa mazingira zinazingatiwa katika kujikinga na Magonjwa ya mlipuko.
“Kwa sehemu kubwa miundombinu ya maji imeathiriwa hivyo wito tunaotoa haya maji yanayotolewa ni kuyatibu ili yawe safi na salama kwa ajili ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko na jamii imeitikia mwito inatumia maji yaliyowekewa dawa ya kutibu maji”amesema.
Halikadhalika amehimiza umuhimu wa utumiaji wa vyoo na kunawa mikono mara kwa mara.
Nao baadhi ya wananchi wamesema elimu ya Afya inayoendelea kutolewa ikiwemo utumiaji wa dawa ya kutibu maji, umuhimu wa kutumia choo,inasaidia wao kujikinga na magonjwa ya mlipuko.