Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imedhamiria kuendeleza mradi wa umwagiliaji katika bonde la Bugwema lililopo wilayani Musoma mkoani Mara ikiwa ni mradi ambao ulianzishwa mnamo mwaka 1974 na hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Hayo yamejiri wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa pamoja na kampuni ya Arab Contractors ya nchini Misri kwa lengo la kukagua eneo la uendelezaji mradi huo wa umwagiliaji.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji amesema nchi ya Misri ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika kilimo cha umwagiliaji hivyo ujio wa kampuni hiyo ya kutembelea bonde hilo ni kuona namna gani bonde hilo linaweza kuendelezwa kwa ubia kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Arab Contractors.
“Tunahitaji kutimiza adhima ya Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta ya Kilimo ndio maana tumekuja hapa kuona namna ya kuhakikisha Shamba hili linakuwa njia sasahihi yakuwasaidia wananchi katika kilimo Bora cha umwagiliaji”Raymond Mndolwa Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
Aidha amesema kuwa ziara hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa sambamba na matumizi ya fedha za serikali katika utekelezaji miradi ya umwagiliaji ni muhimu kuwa na ubia na sekta binafsi katika kuendeleza miradi hiyo.
Mndolwa ameongeza kuwa baada ya upembuzi yakinifu kufanyika katika eneo hilo na iwapo mwekezaji huyo ataridhia kuendeleza bonde hilo wananchi watapata eneo la kulima pamoja na Tume kupata kipato ili kuweza kuendeleza maeneo mengine.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania Bw. Frank Nyabundege amesema benki hiyo itaimarisha ushirikiano kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Kampuni ya Arab Contractors na kuhakikisha mradi huo unaendelea.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Arab Contractors nchini Tanzania Ahmad Suiy amesema wamefikia hatua ya usanifu wa mradi huo na kwamba watahakikisha mradi huo unatekelezeka na kuleta tija kwa Taifa la Tanzania.
Bonde la Bugwema ni miongoni mwa mabonde 22 ya kimkakati ambayo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inafanyia upembuzi yakinifu ambapo mshauri mwelekezi kutoka kampuni ya Mhandisi Consultancy anatarajia kukamilisha zoezi hilo Februari 2024.